Monday, March 12, 2012

Swali kuhusu jina "WAHABIYYA"

Swali: 


Ni nani wahabi? Kwanini waitwe hivyo kama wenyewe wanajiita Salafi?

Jibu:

WAHABI ni yoyote anayefuata itikadi, aqida, harakati na msimamo wa Shehe wa Najidi Muhammad Ibn Abdul-Wahab na kukubaliana nao na kuuendeleza mtizamo huo.



Maulama wengi wa ki-sunni wamewaita hawa watu Wahabi kwa sababu ya jina la shehe wao huyo mkubwa muhuishaji wa dhehebu hilo, Ibn Abdul Wahab. Kuwaita wafuasi wa Ibn Abdul Wahab jina hilo ni kama ambavyo wanaofuata madhehebu ya Imam Shafi' kwa mfano, ambaye jina lake kamili ni Muhammad Ibn Idris Ash-Shafi' huitwa kwa kifupi ma-Shafi'. Wanaofuata dhehebu la Imam Malik huitwa Maliki, Imam Abu Hanifa...Hanafi n.k.

Lakini Mawahabi eti siku hizi hukataa kuitwa hivyo kwa kisingizio kuwa "Wahab" ni katika majina ya Allah. Kwanza katika majina ya Allah ni "Al-Wahab", ikishawekwa AL tu! tunajua anaongelewa nani, hakuna mwingine. Isitoshe yapo madhehebu au makundi tofauti ya waislam yaliyojulikana kwa majina ambayo asili yake inafanana na majina ya Allah: Mfano Maliki, Shafi, Qadiri (Qadriyya) n.k

Hilo linajulikana wazi kuwa kuitwa jina Wahabi/ Wahabiyya ni kutokana na kiongozi wao wanayemfuata. Wanachuoni wa kisunni wamekuwa wakitumia jina hilo, hii inaonyesha uhalali wake kwetu. Kaka yake Ibn Abdul Wahab mwenyewe (Sulayman) aliandika kitabu cha kupinga mtazamo wa ki-wahabi na kukiita "ar-Radd ‘alaa al-Wahhabiyah!"

Tena hata wao wenyewe walilikumbatia jina hilo miaka ya nyuma, na wakijiita hivyo hivyo, walianza kulikana pale umoja wao ulipokuwa na kuenea nje ya mipaka ya Saudia. Uthibitisho unapatikana katika maandiko yao wenyewe. Mawahabi wa bara hindi waliandika kitabu "Tohfa al wahabiyya", (Zawadi kwa mawahabi)!. Mpaka leo hii maandiko ya Sheikh Bin Baz ni ushahidi tosha wa hili, tizama anavyoelezea:

وليست الوهابية حسب تعبير الكاتب بدعاً في إنكار مثل هذه الأمور البدعية، بل عقيدة الوهابية: هي التمسك بكتاب الله وسنة رسوله صلى الله عليه وسلم، والسير على هديه، وهدي خلفائه الراشدين، والتابعين لهم بإحسان، وما كان عليه السلف الصالح، وأئمة الدين والهدى، أهل الفقه والفتوى في باب معرفة الله، وإثبات صفات كماله ونعوت جلاله

Hii ni moja kwa moja kutoka website ya Shekhe huyo mkubwa waliyemfuata huko Saudia (Marehemu), tizama hapa

Kwanini wasiitwe Salafi kama wanavyojiita wenyewe!

Madai yao ni kuwa wao wanafuata vizazi vitatu vya mwanzo katika uislam, yaani Maswahaba, wafuasi wao, na wafuasi wa wafuasi wao (Salaf us Saalih), ambao wanazuoni wengi wamesema waliishi katika miaka mia tatu (karne tatu) za mwanzo. Kwamba "Salafi" ikimaanisha kuwa ni wanaofuata muongozo wa Salaf.

Tunasema ni uongo, kwa sababu mitizamo ya kiwahabi ilianza karne nyingi zilizofuata baada ya vizazi vitatu vyema. Ikumbukwe kuwa Shehe Ibn Abdul Wahab alichofanya ni kuhuisha mtizamo wa Ibn Taymiyyah, lakini si mwanzilishi. Tizama mujadidi wao Shehe Bin Baz anavyoeleza, (Tizama pia anavyotumia jina "Wahabiyya"):

Wahabiyya sio wapya katika kupinga uzushi wote aina hiyo. Akiida yao ni kushikamana imara na Kitabu cha Allah na sunnah ya Mtume wake SallAllahu alayhi wasallam, na kufuata nyayo zake, na za wafuasi wake walioongozwa kihaki. Wahabiyya wanawaamini hao, jinsi walivyoripoti bila ya kugeuza/kubadilisha. Akida ya Wahhabiyya imeelemea katika katika kufanikisha kushuhudia kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Allah na kuwachilia mbali uzushi wote. Huu ndio msingi wa Utawala wa Saudia na huu ndio mtizamo wa wasomi wa Saudi Arabia...."

-- ['Indispensable Implication of the Sunnah and Caution Against Innovation' by Abdul Azeez Abdullah Bin Baz, printed by Ministry of Islamic Affairs, Sa’udi publication no. 385/ page 12-13]

Mengi anayosema si kweli wanayofuata kwani wao ndio wazushi wakuu!, lakini maelezo hayo yanaonesha kuwa fikra na mtizamo wa ki-wahabi vilianza kabla ya Ibn Abd al Wahab. Na ni ushahidi kuwa hata wao wenyewe walijiita WAHABI. Vile vile rejea Tafsir Swawi ya Imam Ahmad Swawi akisherehesha Tafsiri Jalalain , ikiitwa Tafsiri yake Hashiya al Swawi ala Jalalain , angalia chapa zifuatazo Toleo la 1930 chapa ya Cairo (Isa Babi Al-Halabi) Mujarab wa 3 ukurasa wa 255, Pia Toleo la mwaka 1937 chapa ya Cairo (Matabaa Mashhad al Hussein) Mujaraba wa 3 uk wa 307 mpaka 308. Toleo la 1970 chapa ya Beirut(Dar Ihya Turath Al-Arabi) Mujaraba wa 3 Uk wa 307 mpaka 308

Imam Swawi anasema akitafsiri Aya ya 6 sutar Fatwir (Sura ya 35 aya ya 6) anasema: ''Ayah hii inaongelea MAKHAWARIJ ambao watakuja kuharibu Tafsiri za Quraan na Sunnah kama tuonavyo hii leo Hijaz kwa wale tuwajuao kama WAHABIYYAH....'' mwisho wa kunukulu.

Imam Ahmad Swawi hakutumia neno Salafiyah au Muwahidun bali ametumia neno WAHABIYAH ni mfaswaha wa lugha na ndio maana ameandika Tafrisi ya Quraan hata hii leo inatumika na Mawahabi ingawa kwa yale aliyoandika Imam Swawi yamefutwa na viwanda vyao kama tuonavyo matoleo yaliyo chini ya ufadhili wa pesa za petroli kilichochapishwa Beirut na Dar Fikr miaka ya 80 na mwanzoni mwa miaka ya 90 tunaona jina hilo hilo Tafsiri Swawi ila mabadiliko ni mengi mno toka tafsiri ya asili

Mfano Mujaraba wa 3 yale tuliyoyasoma kwenye tafsiri hizo zilizochapishwa miaka ya thelathini na mwanzoni mwa miaka ya 70 hayamo tena hususan--''kikundi hiki tukionacho leo huko Hijaz cha WAHABIYAH ''Haya maneno yamefutwa hayamo tena kwenye tafsiri iliyochapishwa na wao mawahabi

Ukitizama rejea zao nyingi hurudi nyuma mpaka kwa Ibn Taymiyya, unasikia "Shaykh ul Islam alisema hivi" Ingawa wanapinga tunavyofuata madhehebu na kudai wanafuata Qur'an na Hadithi tu, ukweli ni kuwa Mawahabi wanafanya Taqlid kwa Shaykh Ibn Taymiyyah. Tena wanafuata jinsi Ibn Taymiya alivyoamua kutafsiri mambo na kwenda kinyume na wanazuoni wakubwa kabisa wakati wake na kwa karne nyingi kabla yake.

Je, Ibn Taymiyya ni katika Salaf us Saalih?

Ibn Taymiyyah ndiye wa zamani zaidi kati ya mashehe mashuhuri wa mitazamo hiyo, lakini aliishi katika karne ya saba ya kiislam, pamoja na Ibn al Qayyim. Ibn Abd al Wahhab aliishi karne ya kumi na mbili. Wengine mashuhuri waliomfuatia; Ibn Uthaymeen, Bin Baz, na Al Albani wote wameishi karne hii. Wote hao walikuja karne kadhaa baada ya zile karne tatu za mwanzo. Tunaomba Allah awasamehe madhambi yao na udhaifu wao.

Hata tukiacha hoja ya tarehe na namba, mawahabi wameonesha kupingana na Salaf us Salih na Ahlu sunnah wal Jama'a kwenye nyanja tofauti. Mpaka kufikia kuandikwa vitabu na wanazuoni wa ki-sunni kuonya juu ya fitna zao. Vitabu kama ‎"Umara al-Baladil-Haram" kilichoandikwa na mwalimu wa wanazuoni huko Makka, mufti wa ma-Shafii Sheikh Ahmad bnu Zayni Dahlan aliyekufa mwaka 1304 Hijri, "Fitnat ul Wahabiyya" (Fitna ya Wahabiyya), "ar-Radd ‘alaa al-Wahhabiyah!"(kilichoandikwa na kaka yake Ibn Abd al Wahab), na "Ar-Raddu ‘Ala Man qala bil-Jiha" (Tafsiri ya kiingereza).

Ingekuwa haki zaidi kwa wanaofuata madhehebu ya Hanafi, Maliki, Shafi, na hata Hanbali halisi kujiita Salafi (yaani wanaofuata Ma-Salaf wenyewe) kuliko Wahabi kujiita hivyo, kwani maimam hawa wanne wote pamoja na  Abu al Hasan al-Ashari na Abu Mansur Al Maturidi waliishi na kusoma dini katika zama za Tabieen na Taba Tabieen (Karne tatu za mwanzo). Wote ni ma-salaf, na khitilafu zao hazikuwa kubwa kimsingi, bali mambo ambayo hayakuathiri uislam wa jumla wa mtu.

Hatuoni haki kuwalinganisha na Salaf us Saalih, kwa kuwa itikadi zao, jinsi ya harakati zao, na tabia za wengi wao zinafanana zaidi na Ma-Khawarij, na ni mbali na Salaf, kwa hiyo tunapenda kwa heshima kuwanasibisha na Shekhe wao mpendwa kutoka Najdi, ndio maana twawaita WAHABI.

http://www.youtube.com/watch?v=Bt5mwXbdWb0

No comments:

Post a Comment