Tuesday, March 13, 2012

Ujirani katika uislam


Bismillahi Rahmani Rahiim



"Mtumikieni (muabuduni) Allah, na msimshirikishe na chochote; na watendeeni wema wazazi, ndugu, yatima, na wenye shida, majirani walio karibu, majirani wageni, swahiba walio pembeni yenu, wapitanjia (mnaokutana nao), na mikono yenu ya kuume inayomiliki. Hakika Mwenyezi Mungu hapendi wenye kiburi wanao jifakhiri." [Qur'an 4:36]



Uislam haukuacha kumfunza muislam jinsi ya kuishi katika jamii yake. Kuanzia uhusiano kati ya mtu na wazazi wake, mtu na jamaa zake, wapita njia, na hata walio chini yake kimamlaka. Leo hii ningependa tuzungumzie jirani.

Kuishi vizuri na jirani si jambo dogo wala mzaha, ila ni sehemu ya imani ya muislam. Imesisitizwa sana kuishi nao vizuri katika hadithi kadhaa wa kadhaa za Mtume (s.a.w). Moja ya jinsi ya kujenga uhusiano mzuri na jirani ni kuwapa zawadi. Imesimuliwa na Abu Hurayrah (r.a) Mtume amesema: "Enyi wanawake, hata mmoja wenu asidhanie ni jambo dogo kumpa jirani japo zawadi ya kwato za kondoo" [Bukhari]

Imesimuliwa na Aysha (r.a) na Ibn Umar (r.a) kwamba Mtume  wa Mungu (s.a.w) amesema: " Malaika Jibril (a.s) alinihusia mara nyingi sana kuhusu haki za jirani mpaka nikaogopa naye pia (jirani) atahitajiwa kuwa mrithi"

Katika hadithi nyingine iliyosimuliwa na Abu Shurayh (r.a), Mtume (s.a.w) amesema: "Yeyote anayemuamini Allah na siku ya mwisho ni muhimu kwake kutowadhuru jirani zake na  yeyote anayemwamini Allah na siku ya mwisho ni muhimu kwake kuwaburudisha wageni wake kwa wema na ukarimu, na yeyote anayemwamini Allah na siku ya mwisho ni muhimu aongee kilicho chema au vinginevyo abakie kimya"

Hadithi hiyo inaonyesha umuhimu wa muumini wa kweli kuwa makini na jirani zake wakati wote, kuhakikisha  hawaudhi au kuwadhuru kwa namna yoyote. Vilevile inatuashiria jinsi gani Mtume (s.a.w) alizipa umbele haki za majirani. Tizama hadithi nyingine anasisitiza mara tatu Mtume (s.a.w) kuhusu kutowadhuru jirani zetu kama ilivyosimuliwa na Abu Hurayra (r.a): "Wallahi, si muumini wa kweli, Wallahi si muumini wa kweli, Wallahi si muumini wa kweli! Akaulizwa "Nani?" Akajibu, "Ambaye jirani yake hajisikii salama kutokana na uovu wake" Katika hadithi nyingine iliyopokelewa na Muslim, amesema Mtume (s.a.w), " Hatoingia peponi ambaye kwa madhara yake jirani yake hajisikii salama"

Aina na haki za jirani

Katika hadithi iliyosimuliwa na  Jabir (r.a), Mtume (s.a.w) ameripotiwa kusema: "Majirani ni wa aina tatu. Kwanza, jirani anayepata haki moja tu, yeye ni wa daraja la chini. Pili, ambaye anapata haki mbili, na tatu, ni jirani anayepata haki tatu. Jirani mwenye haki moja ni kafiri asiye ndugu. Jirani mwenye haki mbili ni jirani ambaye pia ni muislam, na mwenye haki tatu ni jirani ambaye ni muislam na ndugu (wa damu) - ana haki kama jirani, kama muislam, na kama ndugu."

Amesimulia Mu'awiya Ibn Haidah kwamba Mtume (s.a.w) amesema: "Haki za jirani kwenu ni; anapoumwa mumtembelee (na kumhudumia); akifa mhudhurie mazishi yake; akipatwa na kheri mumpongeze; akipatwa na balaa mhuzunike na kumhurumia; na  muepuke kusimamisha majengo yenu kuwa marefu zaidi ya lake kiasi kwamba hewa safi inazuiwa, na pia kuwa makini harufu ya chakula mnachopika kisimletee huzuni, basi mpelekee kiasi cha chakula hicho." Ana haki zaidi jirani anayeishi karibu zaidi kuliko anayeishi mbali na mtu. Katika hadithi iliyopokelewa na Bukhari na kusimuliwa na Aysha (r.a):  Nikasema, "Ewe Mtume wa Mungu, ninao majirani wawili, yupi nimpelekee zawadi?" Akajibu (s.a.w) "Kwa ambaye mlango wake uko karibu zaidi na wewe"

Utamaduni wetu waafrika mashariki wa kupelekea majirani iftari ni utamaduni mzuri wa kiislam ambao unapaswa kufanyika siku zote, na usiishie mwishoni mwa mwezi huo wa Ramadhani tu. Inatupasa kama waislam tunapopika kuangalia jirani zetu wana hali gani, huenda wameshikwa na njaa siku kadhaa, harufu nzuri ya unachopika yaweza kuwa ni mateso kwao. Tuangalie hadithi hii iliyosimuliwa na Anas (r.a) ambayo Mtume (s.a.w) alisema " Si muumini wa kweli, anayekula na kushiba na kulala bila shida usiku wakati jirani yake ananjaa-huku akifahamu. Basi haidhuru na inapasa kugonga hodi na kupeleka bakuli moja la ulichopika. Hii imeelezwa katika hadithi iliyosimuliwa na Jabir (r.a) ambayo amesimulia kuwa Mtume (s.a.w) amesema ikipikwa gravy (supu/mchuzi) nyumbani kwa mtu basi aongezee majimaji (broth) na apeleke kiasi kwa jirani.

Hazihishii haki katika kuwasaidia na kuwatendea wema kwa mali na hali kwa juu juu tu, bali tunawajibika kuwatendea wema kiroho pia, kuwakumbusha mambo mema na kuwaepusha na mambo mabaya. Waumini na wasio waislam.

Katika hadithi maarufu iliyomo katika Arba'in cha Imam Al Nawawi (Rahimahullah) iliyosimuliwa na Anas Ibn Malik (r.a.), Mtume (s.a.w) amesema: "Hakuna kati yenu anayeamini mpaka anapotaka kwa kaka yake ambacho angekitaka mwenyewe" Wanazuoni wengi wakubwa wa zamani na wa sasa wanasema hadithi hii ni miongoni mwa misingi ya dini yetu (usul al Din). Imam Nawawi, Ibn al 'Imad, Imam Najm al Din al-Tufi na baadhi ya wanazuoni wengine wameitafsiri "anapotaka kwa kaka yake" kumaanisha binaadam wenzetu kwa ujumla (si wanaume pekee wala waislam pekee)

Kwa kuwa tunaamini kuwa uislam ndio njia ya haki na ndio barabara ya kuelekea peponi basi waumini wa kweli wanapaswa kuwaalika majirani wa dini nyingine katika uislam, kwa hekima na busara (da'wah), na kuhimiza na kukumbusha jirani waislam katika heri na kukataza maovu (Amri-bin-ma'ruf Wan-nahyi anil munkar) Vilevile ni vizuri sana kuwaombea Mungu awaongoze katika haki wale ambao bado hawajaiona haki, na kuwaombea kila kheri, na msamaha, walio waislam.

Kama tukitia umakini katika yote yaliyotajwa hapo juu ni wazi kuwa jirani zetu watakuwa wepesi kusikia tunayowaeleza na kuvutwa nayo kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Kwani tayari watakuwa wamejenga heshima, upendo na imani kwetu kutokana na tabia na matendo yetu mema kwao. Kazi ya Daw'ah inakuwa ni rahisi zaidi. Kwa wanaoishi nchi za magharibi mara nyingi ukionyesha ukarimu na wema kama ilivyo katika sunnah mara nyingi watu watakuuliza kwa nini uko hivyo, na ukiitumia vizuri fursa hiyo kuelezea maadili ya dini yetu ni da'wah tosha insha Allah.

Kumbuka kisa cha Mtume (s.a.w) na jirani yake wa kiyahudi. Mwanamke huyo alikuwa na tabia ya uchokozi wa kutupa takataka karibu na nyumba ya Mtume (s.a.w) makusudi kila siku. Siku moja Mtume hakuona takataka pale mahali, akaenda mara moja kuulizia nyumbani kwa yule mwanamke. Bahati mbaya akamkuta ni mgonjwa, akamfanyia ukarimu na kumsaidia. Yule mwanamke akaona aibu na kujisikia vibaya sana.

Huu ni mfano wa hali ya juu wa kuishi kwa wema na jirani zetu.

Wa Allahu 'allam.






No comments:

Post a Comment