Saturday, January 28, 2012

Kwanini msikiti wa Makka ukaitwa Masjid Al Haram?


SWALI:


Neno HARAM na HARAAM yana maana tofauti au ni maana moja tu (kinyume cha halali)? Does it mean "Holy/Sacred" also? Na kwanini msikiti wa Makka ukaitwa Masjid Al Haram?
----------------------------------------------------------------------------------------------

JIBU:

Bismillah, wa Sallah Allah ala Rasul Allah!



Neno HARAM na HARAAM pamoja na meneno mengine ya Kiarabu, yenye mfumo huo huo wa herufi tatu, yaani H + R + M, na ambayo yanatokana na timbuko moja hilo hilo la herufi tatu (thulathiy al-asl) huwa linaamisha: kuzuwia; kukataza; kukatazwa; kupiga marufuku; kutenga mbali; kuepusha; kujiepusha; kutosogelea na kadhalika.

Kwa maana hiyo basi, maneno yote hayo mawili, na mengi mengine yanayotokana na timbuko hilo hilo au mfumo huo huo – iwe kuelezea kitendo au kitenzi, sifa; mtendaji, mtendwaji na kadhalika- huwa na maana hizo hizo, ambazo kinyume chake ni: halali; ruhusa; inajuzu; inakubaliwa; haina kizuwizi na kadhalika. Kwa mfano: Haraam maana yake ni “marufuku” “inakatazwa” na kadhalika. Kile kilichopigwa marufuku huitwa: Muharram, yaani “kimekatazwa” na kadhalika. Aidha, mtu unayepigwa marufuku milele kumuoa au kuolewa naye, kwa sababu ya nasaba ya damu na uzazi au mahusiano ya kunyonya ziwa moja, huitwa: Mahram. Yaani ni mtu ambye kwako ni marufuku milele kumuoa au kukuoa.

Hivyo basi, ni wazi kuwa HARAM na HARAAM hazina maana ya moja kwa moja ya kumaanisha: takatifu au utakatifu na kadhalika, ambayo kwa Kiingereza ni SACRED –kama uylivyotaja-. Na pengine ndiyo ukaona kuwa katika majina 99 ya Mwenyezi Mungu, hakuna jina linalotokana na herufi hizo tatu: h + r + m; kwa sababu katika lugha ya Kiarabu, neno linalotokana na timbuko hilo, halimaanishi Utakatifu.

Naama neno: “takatifu” linawiana na neno la Kiarbu: qadasa au muqaddas au taqdees. Ndiyo basi, mojawapo wa majina ya Mwenyezi Mungu S.W.T ni Quddus: yaani Mwingi wa Utakatifu, Mtakatifu. kwa maana kwamba Hana kosa, wala kasoro, au aibu, au sifa yoyote ile ya upungufu. Mojawapo wa dua muhimu ni ile isemayo: Subbuhu, Quddusu, Rabbuna wa Rabu al-Mala’ikati wa al-Ruh!

Kuitwa msikiti wa Makka: Masjid al-Haram, au Masjid al-Haraam kunatokana na kuwa Msikiti huo umo katika eneo maalum ambalo, tokea hata kabla ya Uwislamu, na baada ya kuja Uwislamu, lilikuwa likijulikana kuwa Bonde lilio Barikiwa (Bakkah Mubarakah), ambalo ndani yake –katika muhula maalum- kunapigwa marufuku na kunakatazwa mambo mbali mbali ya magomvi, vita, kupigana, kugombana, kuua, kulipizana kisasi na kadhalika. Yote hayo ni haramu kuyatenda katika eneo hilo na katika muhula huo. Uwislamu uliendeleza maana hiyo na kuiwkea taratibu maalum kuhusu eneo hilo, miezi hiyo na ibada inayotakiwa kufanywa katika kipindi hicho. Ndiyo maana eneo lote la Makka, ambalo mipaka yake inajulikana, limeendelea kuitiwa kuwa ni eneo la al-Haram au al-Haram.

Vile vile, kabla ya Uwislamu, Maqureshi na waarabu wengine walikuwa wakienda katika eneo hilo, kila mwaka kwa madhumuni ya kutufu al-Kaaba katika msimu huo. Kwa vile ni tendo linalofanyika kila mwaka, katika kipindi maalum, basi likawa tendo hilo linaitwa Hijja: yaani Makusudio. Jinsi walivyokuwa wakiheshimu al-Kaaba, wale waliokuwa wakienda kuhiji wakitwa: Haajj au Hujjaaj (mwanamke Haajah) Aidha, mahujaji wa kipindi cha Ujahiliyya, walikuwa wakivua nguo zao zote na kuwa uchi – uchi wa nmnyama- wakti wa kutufu; kwani walikuwa wakiamini kuwa nguo zao ni chafu au zimepatikana kutokana na mambo machafu! Walikuwa wakizivua na kuziweka kando. Nguo hizo wakiziita: Hurm au Hirm: yaani nguo zilizotengwa zisiguswe wakti wa kuhiji.

Uwislamu ulipokuja na kuondoa masanamu yote yaliyokuwa yakiabudiwa na Maqureshi na kugeuza eneo la al-Kaaba kuwa ni msikiti, uliendeleza jina la eneo hilo kuwa ni al-Haram na msikiti huo ukaitwa: Masjid al-Haram au Masjid al-Haraam. Ibada ya Hija, iliyowekewa utaratibu wake maalum na ikawa mojawapo wa nguzo Tano za Uwislamu, kwa mwenye kuweza kwenda safari hiyo, mara moja katika maisha yake. Pia ukaweza taratibu maalum, tofauti na zile za Maquresh waliokuwa wakitufu uchi, kuwa ndio taratibu maalum za Kuhiji. Waislamu wakatakiwa kuvaa vazi maalum, ambalo halikushonwa na ambao linaitwa: Ihraam; yaani vazi la kuhijia na ni vazi linaloonesha kuwa aliyevaa Ihraam ni Muhrim na yumo katika eneo la Haram, katika kipindi cha Hurum, na kadhalika. Aya zifuatazo zinatoa ufafanuzi mzuri zaidi kuhusu hayo niliyoelezea hapo juu.

قال الله عَزَّ و جَلَّ : ﴿ إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ وَقَاتِلُواْ الْمُشْرِكِينَ كَآفَّةً كَمَا يُقَاتِلُونَكُمْ كَآفَّةً وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ ﴾ [2] .
و قال تعالى: ﴿ يَسْأَلُونَكَ عَنِ الشَّهْرِ الْحَرَامِ قِتَالٍ فِيهِ قُلْ قِتَالٌ فِيهِ كَبِيرٌ وَصَدٌّ عَن سَبِيلِ اللّهِ وَكُفْرٌ بِهِ وَالْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَإِخْرَاجُ أَهْلِهِ مِنْهُ أَكْبَرُ عِندَ اللّهِ وَالْفِتْنَةُ أَكْبَرُ مِنَ الْقَتْلِ وَلاَ يَزَالُونَ يُقَاتِلُونَكُمْ حَتَّىَ يَرُدُّوكُمْ عَن دِينِكُمْ إِنِ اسْتَطَاعُواْ وَمَن يَرْتَدِدْ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَيَمُتْ وَهُوَ كَافِرٌ فَأُوْلَئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ وَأُوْلَئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴾ [3] .
و قال جَلَّ جَلالُه: ﴿ فَإِذَا انسَلَخَ الأَشْهُرُ الْحُرُمُ فَاقْتُلُواْ الْمُشْرِكِينَ حَيْثُ وَجَدتُّمُوهُمْ وَخُذُوهُمْ وَاحْصُرُوهُمْ وَاقْعُدُواْ لَهُمْ كُلَّ مَرْصَدٍ فَإِن تَابُواْ وَأَقَامُواْ الصَّلاَةَ وَآتَوُاْ الزَّكَاةَ فَخَلُّواْ سَبِيلَهُمْ إِنَّ اللّهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴾ [4] .
و قال عَزَّ مِنْ قائل: ﴿ الشَّهْرُ الْحَرَامُ بِالشَّهْرِ الْحَرَامِ وَالْحُرُمَاتُ قِصَاصٌ فَمَنِ اعْتَدَى عَلَيْكُمْ فَاعْتَدُواْ عَلَيْهِ بِمِثْلِ مَا اعْتَدَى عَلَيْكُمْ وَاتَّقُواْ اللّهَ وَاعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ ﴾ [5] .
و قال سبحانه و تعالى: ﴿ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ لاَ تُحِلُّواْ شَعَآئِرَ اللّهِ وَلاَ الشَّهْرَ الْحَرَامَ وَلاَ الْهَدْيَ وَلاَ الْقَلآئِدَ وَلا آمِّينَ الْبَيْتَ الْحَرَامَ يَبْتَغُونَ فَضْلاً مِّن رَّبِّهِمْ وَرِضْوَانًا وَإِذَا حَلَلْتُمْ فَاصْطَادُواْ وَلاَ يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ أَن صَدُّوكُمْ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ أَن تَعْتَدُواْ وَتَعَاوَنُواْ عَلَى الْبرِّ وَالتَّقْوَى وَلاَ تَعَاوَنُواْ عَلَى الإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ وَاتَّقُواْ اللّهَ إِنَّ اللّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴾ [6] .
و قال عَزَّ و جَلَّ: ﴿ جَعَلَ اللّهُ الْكَعْبَةَ الْبَيْتَ الْحَرَامَ قِيَامًا لِّلنَّاسِ وَالشَّهْرَ الْحَرَامَ وَالْهَدْيَ وَالْقَلاَئِدَ ذَلِكَ لِتَعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ وَأَنَّ اللّهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴾ [

Kwa ufupi, Haram au Haraam au al-Haram au al-Haraam au Muhrim au Muhrima ni majina yenye uhusiano wa maana hizo nilizozitaja awali, hapo juu kabisa na hazimaanishi moja kwa moja na utakatifu (sacred).

Hata hivyo, kwa upande wa matumizi ya kawaida (istilahi), na hasa katika lugha nyengine zisizohusiana sana na Kiarabu, kama vile Kiswahili na Kiingereza, yumkini pia lugha nyingi nyengine, ile hali ya mtu kuzuwiliwa au kukatazwa kufanya mambo mbali mbali, katika eneo hilo liliopigiwa marufuku vitendo hivyo, na katika muhula huo maalum, hali hiyo ya upigwaji marufuku imepelekea kuielezea hali hiyo kwa kutumia maneno kama: takatifu au visawe vyake. Ndiyo maana, tukawa tunasikia katika Lugha ya Kiswahili, mashekhe wetu wanasema: Miezi mitakatifu, Msikiti mtakatifu na kadhalika, wakimaanisha miezi iliyotukuzwa kwa kupigwa marufuku kufanya vitendo maalum na kadhalika. Vivyo hivyo, wanaposema: Msikiti mtakatifu, huwa wanaaamisha hayo hayo. Hii inajuzu katika lugha, ilimradi tu maana iwe ni hiyo ya kuheshimiwa zaidi na kutukuzwa na SI UTAKATIFU, kwa maana ya UTUKUFU ULIOTUKUKA, USO KASORO WALA WALAKINI. Hiyo ni sifa ya Mjwenyezi Mungu S.A.W., ambaye hana mshirika wala hakuna kitu mfano Wake. Jalla Jalaluh!

Wa billahi al-tawfiq

Dr. A. Shareef.


No comments:

Post a Comment