Saturday, January 28, 2012

Zanzibar Muslim Academy --1960's




Kutoka kulia kwenda kushoto: Waliokaa: wa kwanza ni Sayyid Ahmad Hamid Mansab Ibn Shaykh Abi Bakr bin Salim (alikuwa akisomesha Nahw, na Sarf); wa pili kutoka kulia ni Al-ällama alkabir Sheikh Sulaiman bin Muahammad Al-Alawi - huyu bwana ni mwalimu wa karibu maulamaa wote wa Zanzibar na nchi jirani za Afrika ya Mashariki- alilkuwa bahari isiyo na fukwe kwenye elimu mbali mbali. Yeye alisomesha Fiqh; Arudhi (elimu ya fani ya kutunga mashairi ya Kiarabu); Balagha na kadhalika. Ni shida, kama si muhali, kumpata mwana chuoni ye yote katika Afrika ya Mashariki, Kati na Kusini, asiwe mwanafunzi wa Maulana huyu: Allah yarhamhu. Maisha yake yote yalikuwa katika kusomesha dini tu, tokea anaamka hadi anakwenda kulala. Msikiti Gofu ulikuwa ndio mahali anaposomesha kuanzia baada ya sala ya Alfajiri, hadi baadaye kwenda Muslim Academy, na akirudi baada ya sala ya Adhuhuri hadi baada ya sala ya Isha. Allah yarhamhu wa yuskinuhu al-Janna.

Wa tatu kutoka kulia na Sayyid Umar bin Abdallah Ibn Shaykh Abi Bakr bin Salim (Mwinyi Baraka). Yeye alikuwa Mwalimu Mkuu wa Muslim Academy. Wa nne kutoka kulia ni Sayyid Abdurrahman bin Hamid Al-Sirry - Huyu Bwana alikuwa bahari katika elimu za Lugha, Mashairi na fani nyengine. Yeye alisomesha Arabic Literature (al-Adab al-Arabiyy).

Wa tano kutoka kulia ni Sayyid Ali Badawi Jamalullayl- huyu Bwana alikuwa alim mkubwa sana. Alisomesha Jiographia ya Nyota, Sayari na Ardhi. Vile vile alisomesha Elimu ya Maani na Balagha.

No comments:

Post a Comment