SWALI:
Hivi kila mara tunazungumzia kukaa eda!
Je hiyo Edda inakaliwa vipi?
Nini masharti ya Edda au kuna mavazi maalum ambayo yanatakiwa kuvaliwa??
Je kunatofauti ya hizi edda mbili ( ya kufiwa na kuachwa) zaidi ya kupishana siku kama mwanamke si mjamzito??
Naombeni kufahamishwa kiundani juu ya hili tafadhali! :
-----------------------------------------------------------------------------------------------
MAJIBU, kwa muhtasari:
Eda ni muhula maalum aliouweka Mwenyezi Mungu, kwa mwanamke aliyefiwa na mumewe, katika ndoa halali, au aliyetalikiwa ndani ya ndoa halali. Muhula huo ama ni wa uja uzito, au Tohara za hedhi, au miezi.
Hivyo, sababu ya Eda ni mbili; 1. Kufiwa na mume au 2. Kuachwa kwa talaka.
Katika muhula huo, mwenye kukaa eda, iwe ya kufiwa na mume au kuachwa anakatazwa mambo mawili makuu. A) Kuolewa upya 2)Kuposwa; mpaka baada ya kumalizika muhula wa eda.
Mfiwa na mume, hata hivyo, ana nyongeza ya mambo anayokatazwa kufanya. Nayo ni kujiepusha na kila jambo ambalo linaweza kuchangia kuwavutia wanaume wengine kutaka kumuoa au kumposa. Kwa maana hiyo, haruhusiwi kujipamba (kama kuvaa dhahabu na vitu vengine vya mapambo) , kujirembaremba kuonesha uzuri wake, ikiwa pamoja na kujitia wanja wa macho kwa lengo la kupendeza (kutia rangi ya midomo, kw mfano), kujitia manukato ( ikiwa pamoja na kujifukiza nyudi za harufu nzuri nzuri) na kutoka nje ya nyumba anayokaa eda, pasipo na sababu ya msingi.
Ukiacha hayo makatazo ya hapo juu, mkaa eda anaendelea na maisha yake ya kawaida, kama mwanamke yeyote mwengine; ikiwa pamoja na kukoga kama kawaida yake, ikiwa pamoja na kutumia sabuni za kuogea ambazo alikuwa akizitumia kabla, kukinga harufu mbovu mwilini mwake (kama kutumia deodorant kwapani, au kujisafisha damu ya hedhi kwa vitu vinavyoondoa harufu mbaya ya damu hiyo, na kadhalika), kuosha nywele zake kama kawaida yake, kuvaa nguo safi, kuvaa viatu kama kawaida yake, kufua nguo zake, kula chakula akitakacho cha halali, kukutana na wote ambao ilikuwa halali kwake kukutana nao uso kwa uso, kabla ya kuingia katika muhula wa eda. Maana Eda SI kifungo cha jela wala cha nyumbani; bali ni muhula maalum wenye lengo la kutakasa fuko la uzazi, au kutatafakari upya –hasa kwa mume aliyemuacha mkewe- kuhusu athari za kumuacha mkewe na hivyo kuweza kubadilisha maamuzi yake ya awali, au –kwa aliyefiwa na mumewe, kuwa katika huzuni ya kuondokewa na mumewe na hivyo watu wengine waheshimu hali yake hiyo na wasimbughudhi kwa kutaka kumuoa au kumposa.
Mahali pa kukaa eda ni ndani ya nyumba ya mume, kadiri iwezekanavyo, iwe eda ya kuachwa au eda ya kufiwa. Na katika muda wote huo, mwenye kukaa eda anaendelea kulishwa na mume mtaliki, au kutokana na mali ya marehemu mumewe, hadi eda yake ishe. Kwa maneno mengine: Chakula na Malazi ni juu ya mume mtaliki, au kutokana na mali ya marehemu mume –iwapo urithi hautagawanya kwa wahusika, kizuka akiwa mmoja wa warithi.
Kuhusu eda ya mfiwa, Mwenyezi Mungu anasema:
[ وَالَّذِينَ يُتَوَفَّوْنَ مِنكُمْ وَيَذَرُونَ أَزْوَاجاً يَتَرَبَّصْنَ بِأَنفُسِهِنَّ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَعَشْراً ]( البقرة : 234 ) .
Na wale wanaofishwa miongoni mwenu na kuacha wake, basi wake hao watajikalia eda wenyewe miezi mine na siku kumi.
Hali kadhalika Mtume amesema:
وقوله صلى الله عليه وسلم : « لا يحل لامرأة تؤمن بالله واليوم الآخر أن تحد على ميت فوق ثلاث ليالٍ إلا على زوج أربعة أشهر وعشراً »
Haijuzu kwa mwanamke anayemuamini Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho “ amuomboleze” maiti zaidi ya siku tatu, isipokuwa “ kumuombolezea” mume kwa muda wa miezi mine na siku kumi”.
Ama mja mzito, basi eda yake inaisha mara tu baada ya kuzaa.
[ وَأُوْلاتُ الأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ ]( الطلاق : 4 )
Kinyume na Mfiwa, Mtalikiwa (mke aliyeachwa) anaruhusiwa kujipamba, kujiremba na kujipendekeza kwa mtaliki wake (mume wake), maana katika kipindi chote hicho cha eda, ndoa yao bado haijakatika moja kwa moja, na hivyo basi, endapo mume atamrudia kwa kauli au kwa kitendo – kama kumuingilia kimwili- basi eda inakatika na anarudi kuwa mkewe tena. Ila talaka moja imeshapita.
Mfiwa, kwa upande wake, haruhusiwi kujipamba pamba, kujipodoza, kujifukiza, kujitia manukato na kadhalika; mambo ambayo yanaweza kuwavutia wengine kutaka kumuoa. Kwa maana hiyo, hatakiwi kuwa mchangiaji mkuu wa kuwavutia wengine; bali kuonesha huzuni yake. Hivyo, haruhusiwi, kwa mfano, kwenda maharusini, na anatakiwa apitishe muhula wa eda yake kwenye nyumba ya marehemu mumewe, kadiri iwezekanavyo, ikiwa haiwezekani basi kwa wazee wake mwenyewe mwanamke.
Mwanzo wa Eda.
Eda ya kuachwa inaanza mara tu baada ya kutalikiwa, iwe kwa maneno au kwa maandishi, na SI wakati au siku ya kumfikia habari ya kutalikiwa. Vile eda ya mfiwa inaanza BAADA ya kumfikia habari ya kifo cha mume wake na SI mara tu baada ya kufa mume.
Kutokaa eda ni HARAMU, na kuchelewesha eda kwa sababu zisizo za msingi, hasa baada ya kupata habari ya kufa kwa mume, ni haramu vile vile. Kwa maana hiyo, EDA ni wajibu.
Mwenye kukaa eda anaruhusiwa kutoka nje ya nyumba ya eda –nyumba ya mume- kwa haja zake za lazima; mfano kwenda sokoni iwapo hana mtu wa kumtuma, kwenda kazini iwapo analazimika kwenda kazini, iwe alikoajiriwa au alikojiajiri mwenyewe. Jabir R.A. amesema:
حديث جابر بن عبد الله - رضي الله عنه - قال : طُلّقت خالتي فأرادت أن تَجُدَّ نخلها ، فزجرها رجل أن تخرج ، فأتت النبي صلى الله عليه وسلم فقال : « بلى ! فجُدّي نخلك ، فإنك عسى أن تصَدَّقي أو تفعلي معروفاً
“Khaloo (mama mdogo) wangu alitalikiwa. Akataka kutoka kwenda kupalilia shamba lake la mitende. Mtu mmoja akamkemea asitoke! Mama mdogo akamuendea Mtume S.A.W. na kumuuliza. Mtume S.A.W. akasema: Siyo kweli! Nenda ukapalilie mitende yako; kwani huenda ukatoa sadaka au kutenda wema (kutokana na vuno la shamba lako). “
Kwa maana hiyo, mtalikiwa au mfiwa, anaweza kwenda kazini, masomoni, hospitali kwa matibabu, sokoni iwapo hana wa kumtuma, na iwapo ana ukiwa nyumbani basi anaweza kwenda kwa ndugu zake nyakati za mchana kwa kujiondolea ukiwa na unyonge.
Mavazi.
Eda haina mavazi maalum, wala mavazi ya rangi maalum, wala chakula maalum, wala mahali maalum ndani ya nyumba anayokaa eda. Anaendelea kuvaa nguo zake za kawaida, za rangi zake za kawaida, na anakula chakula cha kawaida, na anatembea na kukaa sehemu yoyote ile ndani ya nyumba ya eda. Hali kadhalika, watu wote ambao alikua akionana nao uso kwa uso, kabla ya eda, yaani maharilm wake, anaendelea kuonana nao kama kawaida. Eda SI KIFUNGO!
Wala hakuna sherehe au maombolezo maalum ya kutoka Eda! Unapomalizika muhula wa eda ndiyo eda imekwisha. Sana sana, mtu anaweza kufanfya kisomo kumshukuru Mwenyezi Mungu S.W. kwa mtihani alioumpa na kufaulu kwake mtihani huo na kumuomba afya njema, umri mrefu na maisha bora kuliko alikuwa nayo kabla ya eda. Anaweza vile vile, mfiwa, kumuombea mumewe maghfira na rehema baada ya kutoka eda kwa kusoma dua au kutoa sadaka kwa masikini. Lakini, kimsingi, hakuna TUQUS –taratibu za kutoka eda zaidi kuliko kuwa eda ikimalizika ndiyo imemalizika na yale ambayo alikuwa akikatazwa kuyafanya, sasa anaweza kuyafanya, ikia pamoja na kuposwa upa au kuolewa.
Natumai nimejibu maswali yako yote. Iwapo bado panahitajika ufafanuzi niarifu. Wa Billah al-Tawfiq Dr A Shareef
As salaamu alaikum! Shukrani na sifa zote ni zake Allah [Subhanahu Wa Ta'allah]; rehma, baraka, na amani za Allah zimfikie kipenzi wetu Mtume Muhammad [Sallalahu alayhi wasallam], ahli zake, swahaba wake, na wanaomfuata. Dhumuni la Blog hii ni kukumbushana, kuelimishana na kusambaza mafunzo ya ilm tasawwuf/tazkiyah, iliyojengeka juu ya msingi wa Qur'an na Sunnah haswa kwa kufuatana na madhehebu ya Imam Shafii.
Search This Blog
Thursday, January 26, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment