Friday, February 3, 2012

Hukmu ya kusherehekea Mazazi ya Mtume swallahu aleihi wa salaam


Bismillah alRahman alRahiym


Kwa mujibu wa mafunzo ya kiislamu ni muhimu (bali ni wajibu) kuyaelewa mas-ala kabla ya kuyatolea hukumu. Wanachuoni wa Usuul wanasema kuelewa mas-ala ni nusu ya jawabu. Nasi kabla ya kutoa hukumu juu ya mas-ala ya maulidi ni vizuri tukawa na mtazamo sahihi juu ya kadhia nzima kabla hatujatoa hukumu. Quran inatuonya kuwa kusema kuwa hili ni halali na hili
ni haramu bila ya kuwa na elimu ni kumzulia Mungu, na hili litapelekea katika adhabu kali mbele ya Mungu.
Kimsingi Maulid ni kumsherehekea Mtume swalallahu aleihi wa salaam  kwa ujumla na hususan kusherehekea mazazi yake. Hii ndiyo nadharia ambayo tunaiangalia, na kwa ujumla sherehe hizi zinachukua sura mbalimbali, katika miji na nyakati tofauti. Hivyo swala lililoko mbele yetu ni kuona kamajambo hili linafaa au linakubalika kisheria au la.
Katika kulijibu swali hili kwanza napenda nikubaliana na baadhi ya wapinga maulid kuwa baadhi ya mambo yafanyikayo katika baadhi za sherehe za maulid, ni haram na mara nyingi huwa yanakemewa na baadhi ya masheikh wakati wa hizo maulid. Mfano ni kuchanganyika wanaume na wanawake, katika baadhi miji wakati wa mawlid, sidhani kama yuko mtu atakayejuzisha hilo...
Naam, tukirudi katika mas-ala yetu ya msingi nitatoa hoja katika makala hii, (japo kwa ufupi) kuonyesha kuwa swala hili kama lilivyo katika mfumo wa sasa ni kweli halikuwepo wakati wa mtume, lakini kutokuwepo kwake hakulifanyi kuwa ni baya na haramu. Hii ni kwa sababu  sio kila ambacho hakikuwepo wakati wa Mtume kinakuwa hakifai. Sote tunajua kuwa kuna mambo mengi ya kidini ambyo hayakuwepo wakati wa Mtume lakini kutokana na umuhimu wake na kwa vile yalivyo na mashiko sahihi ya kidini basi yalikubaliwa na wale waliokuwepo wakati ule na yakawa ni sehemu ya dini. Nitatoa mifano baadaye...
Lakini kwa sasa napenda nionyeshe kuwa kuwa kuna misingi ya kidini inayofanya swala zima la maulid liwe ni lenye kukubalika na ni sehemu ya dini. Nitatoa hoja kutoka katika Qur'an na Sunna na hoja za kiakili na kilugha kuthibitisha usahihi wa madai yangu. Baadaye nitaonyesha japo kwa uchache udhaifu wa hoja za wale wanaokana Maulid kuwa ni sehemu sahihi ya dini.
Katika Surat Yunus aya ya 58, Allah anasema: ''Sema: 'Kwa fadhila za Mwenyezi Mungu na kwa rehema zake .... Basi na wafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hivyo wanvyovikusanya' ''. Hoja hapa ni kuwa kupatikana kwa rehema na fadhila za Allah ni sababu kubwa kwa waumini kufurahi. Pia hili la kufurahi na kufanya sikukuu kwa ajili ya kushukiwa na aya ya MwenyeziMungu na rehema zake na fadhila zake limetajwa tena katika Surat al Maidah aya ya 114, kwenye dua ya nabii Isa ya kuomba chakula kutoka mbinguni '... ile kiwe sikukuu...' Kwetu sisi waislamu hakuna rehema na fadhila kubwa kutoka kwa Mungu na aya kubwa ya Allah kwa wanadamu zaidi ya majilio ya Mtume. Na Maulid ni moja ya namna ya kuonyesha furaha yetu kwa hilo.
Allah anasema لقد مَنّ الله على المؤمنين إذ بعث فيهم رسولاً من أنفسهم
"Na Allah amewafanyia fadhila waumini kwa kuwapa mtume toka miongoni mwao"
Tunaona pia katika vitabu vya hadith Mtume swalallahu aleihi wa salaam  alipofika Madinah alikuta Mayahudi wakifunga mwezi kumi Muharram , akauliza kwa nini wao wamechagua siku hiyo kufunga? , wakajibu kwa kusema ni siku ambayo Allah alimwangamiza Fira’un na akamuokoa Nabii Musa(A.S), hivyo tunafunga siku hii kumshukuru Allah Subhanahu wa Taalah kwa neema alizotujaalia Allah   ambayo kishariah inaonyesha uhalali wa kumshukuru Allah(S.T).Hoja hii imetumiwa na Muhadith Hafidh Ibn Hajar Al Asqalani kutetetea maulid. Sisi waisilamu tunasheherekea  kwa siku tuichaguayo , au msimu Fulani katika kila mwaka kwa njia nyingi za ibada kama vile kusoma Quraan na dhikr(hadhara) , kuswali , kufunga , kujitolea na kufanya swadaqa.Kwetu sisi Mtume swalallahu aleihi wa salaam  ni Rahma kubwa ambayo yatufaa kuisherehekea siku aliyozaliwa kama alivyofanya yeye kwa kufunga sisi ambao hatukumuona Mtume swalallahu aleihi wa salaam  tufanye nini?.
Na katika hadithi sahihi ya Mtume swalallahu aleihi wa salaam  juu ya sababu ya kufunga Jumatatu, akasema kuwa hiyo ni siku aliyozaliwa. Hii ni ishara ya wazi juu ya umuhimu wa siku ya kuzaliwa mtume swalallahu aleihi wa salaam  , na kwamba katika kumfuata mtume swalallahu aleihi wa salaam  juhudi za wazi ni lazima zifanyike kumshukuru Mungu juu ya hilo. Maulid ni miongoni mwa juhudi hizo.
Mara nyingi kuna hoja inajengwa kuwa kama jambo halikufanyika wakati wa Mtume basi hakuna ruhusa ya kufanya jambo hilo. Hoja hii ni dhaifu kwa sababu sote tunajua kuna mambo' mengi ya kidini' ambayo hayakufanyika wakati wa Mtume swalallahu aleihi wa salaam  lakini masahaba au wale waliokuja baada yao waliyafanya na yalihesabiwa kuwa ni sehemu ya dini.
Mfano mzuri ni swala ya taraweh, ambayo ni sehemu ya dini na ambayo imekuwa ikiswaliwa miaka yote na waislamu tokea zama za Khalifa Umar (r.a) na hakuna muislamu aliyesema kuwa hilo halifai, bali Umar alinikuliwa akisema kuwa hii ni BIDAA NZURI. Hoja kuwa Umar alikusudia Bidaa ya kilugha ni dhaifu kwa sababu tunajua kuwa bidaa aloikusudia ni watu kuswali tarawehe jamaa na hili ni swala la kidini na sio swala la kilugha.
Imesimuliwa katika Sahihi Bukhari mujaraba wa 3, juzuu 32, hadithi namba 227:  kuhusu  Bida’a;
'Abdur Rahman bin 'Abd ul-Qariy anasimulia, " Nilikuwa na  Umar bin Al-Khattab  usiku mmoja katika masiku ya Ramadhan msikitini tukakuta watu  wakiswali katika makundi tofouti tofauti wengine wakiswali kivyaovyao(pekee yao) na wengine kwenye kigenge kidogo cha watu  chini ya Imam  mmoja, Sayidna Umar akasema, "Kwa rai yangu ningependa kuwakusanya hawa watu wote  wakasali chini ya Imam mmoja na hivyo wasali chini ya imam huyo.
Siku iliyofuata alipowakuta wanaswali kwa pamoja akafurahi na kusema…..نِعْمَت البِدعةُ هذِه
Kwa mtazamo na mujibu  wa skuli ya Kisalafiyah  nafikiri hii ni bidaa ya "kilugha’’ hata sielewi wanakusudia nini kusema hivyo. Kwa kitendo hiki na kauli ya Sayidna Umar (R.A) uwelewo  na mtazamo wa wa  Ibn, ni hawa watu wanaosema kuwa bidaa haigawanyiki kivyovyote leo hii wakibanwa husema bidaa ya Kilugha!!!Hebu tusome wafaswaha wa lugha na Hadith wanasemaje kuhusu neon hili alilolitumia sayidna Umar (Radhiallahu anhu)
Hajar Asqalani  katika sherhe yake  ya swahih al Bukhari anasema ya ama maneno haya Sayidna Umar (R.A).... (Ni’mat al bida hadhihi)……
Anasema hivi;
Asili ya neno bidaa ni kile kilichokuja baada ya mtume swalallahu aleihi wa salaam  Ni moja katika kanuni za kishariah kwa jambo lenye kuendana kinyume na Sunnah na hivyo kuwa dhwalala. Kimsingi jambo hilo kama likiwa ni zuri kisharia basi linakuwa bidaatul Hassana, kama jambo hilo likiwa  halikubaliani na shariah basi linakuwa mustaqbaha, vilevile kama litakuwa linakubalika na baadhi linakuwa Mubah.

Vilevile Bidaa 
inaweza kugawanyika katika vipengele vitano. Hapa Ibn Hajar hajatuletea hoja za bidaa ya Kilugha bali jinsi anavyoelewa neno Bidaa.
Kilichotokea hapa ni kuwa Umar alianzisha mwenendo mwema na hivyo yeye na maswahaba wengine waliohusika wataendelea kupata malipo yao mpaka siku ya kiyama, kama ilivyo katika hadithi nyingine ya Mtume swalallahu aleihi wa salaam 

من سنّ في الإسلام سنّةً حسنة فله أجرها وأجر من عمل بها بعده من غير أن ينقص من

أجورهم شىء، ومن سنّ في الإسلام سنّة سيئة كان عليه وزرها ووزر من عمل بها من

بعده من غير أن ينقص من أوزارهم شىء.
Hadithi inasema: "Atakayeanzisha mwenendo mwema "سُنَّةً حَسَنَةً katika Uislamu atapata ujira wake na ujira wa atakayetenda wema huo hadi siku ya Qiyaamah bila ya kupungua kitu katika ujira wa waliotenda, na atakayeanzisha mwenenedo mbaya سُنَّةً سَيِّئَةً atapata madhambi yake na madhambi ya atakayetenda madhambi hayo mpaka siku ya Qiyaamah bila ya kupungua kitu katika madhambi yao." (Swahih al- Muslim na At-Tirmidhy na An-Nasaaiy na wengine) 
Sasa tuawaulize wale wanaonadi kila bidaa ni upotofu na vipi je kuna Sunnah mbovu waijuayo?hadith hii huiruka sana na kujifanya hawaitambui au kuwa hap si mahala pake. Bidaa nyingine tuipatayo kwenye vitabu vya Sunnah.



Mbali na Tashahud ya kawaida tuijuayo  Abdullah Ibn `Umar. Alifanya nyongeza katika  mwanzo wa Tashahud (Tahiyatu) kwa kuanza kusema (Basmallah) yaani Bismillah Rahman Rahim, na mwisho akaongeza Talbia; "labbaika wa sa'daika wal khayru bi yadayka wal raghba'u ilayika wal `amalu" Haya yameelezwa katika Bukhari na Muslim.
Baadhi ya Bidaa njema za miaka  ya hivi  karibuni:

  • Watu kukusanyika katika misikiti miwili mitukufu ya Makkah na Madinah  na misikiti mingi duniani kuswali Tahajud baada ya salat Taraweh nyuma ya Imam mmoja (wakibadilisha na wasomaji mara nyingi)
  • Kusoma dua ya kukhitimisha Quraan katika swala ya Taraweh na vilevile katikaTahajud mwezi wa Ramadhan!

  • Kufanya mwezi 27 siku ya kukhitimisha Quraan katika misikiti miwili Makkah na Madinah
  • Muadhin kusema maneno Allah akulipeni  malipo mema(bora), baada ya kumaliza Taraweh na Qiyam katika misikiti miwili ya Makkah na Madinah


Hatuyakatai haya kwani twajua msingi wake ni Bidaa iliyo nzuri , ila twasema kuwa
wale wapingao Maulid , hakika hawajioni na hujifunga wao wenyewe dhidi ya  kauli zao wenyewe kwa kusema kuwa kila ambalo hakulifanya Mtume S.A.W au swahaba zake ni upotofu, kwa mantiki hii basi wao pia wako katika upotofu kwa kuanzisha haya na mengineyo...
Au Bidaa hizi ni za ‘’Kilugha(lughawiyah)?
 Maana ya  كُلُّ بِدعةٍ ضَلالةٌ:
Hafidh  Ibn Hajar Al Asqalani, aliyefanyia sherhe   Al Bukhari,  anatuambia  kuhusu bidaa, " Chochote kile ambacho hakikuwepo wakati wa mtume S.A.W kinaitwa Bida’a lakini kuna Bida’a njema na Bida’a mbaya. Abu Na'im, anasimulia kutoka kwa  Ibrahim Al Junaid, asema , "Nimemsikia  Ash-Shafi'i anasema, "Bida’a zipo za aina mbili , bida’a njema(hasana) na chochote kile kitakataana na Sunnah ni dhwalalah(ni bida’a mbaya) na bida’a mbaya (dhwalala)
Suali linakuja Maulid yapingana na  na  Quraan na Sunnah?
Al-Hafidh al Bayhaqi, Manaqib As-Shafiy(1: 469)
"Al Muhadithatu min umuri darbani alduhuma ma uhitha yukhalifu kitaban aw sunatan aw atharan aw ijma’an fa hadhihi al bidaatul dhalala wal althaniyatu ma uhdidha min khairi la khilafa fihi li wahidin min hadhihi wa hadhihi muhdathatun ghayru madhmuma"
Imam Albayhaqi anasimulia katika  Manaqib Ash-Shafi'i ya kwamba  Ash-Shafi'i  anasema kuwa , Bidaa zipo za aina mbili , ile ikataanayo na Quraan na Sunnah(Bidaa’t dhalala)  na Bidaa nzuri ni ile ambayo haipingani na hivi(yaani Quraan na Sunnah) 
Al `Izz bin Abdussalam anasema mwisho wa kitabu chake ,  Al Qawa'id,
Bidaa imegawanyika katika  ulazima, ilokatazwa , inayopendekezwa, isokubalika na inayokubalika, na ukitaka kuifahamu basi angalia ile inayopishana na shariah (Quraan na Sunnah)
Pamoja na kwamba iliwachukua waislamu takriban karne nne kuzinduka kuhusiana na swala hili la maulid, hiyo siyo hoja kuwa jambo hilo linakwa haram, kwani kuna rekodi sahihi za wanachouni wengine kabla ya hapo kujihusisha kwa namna moja au nyingine kumsifu mtume na kumshangilia, hivyo maulid yanakuwa ni maendeleo mwafaka katika mrengo huu. Na hata wale wanachuoni waliokuja baadaye wanaohesabiwa kuwa ni wanachuoni wa mrengo wa ki-salaf, pia walijihusisha na maulid kwa kuandika vitabu n.k kuonyesha kuwa swala hili halipingani na mafunzo sahihi ya Mtume.
Sheikh Ibn Taymiah  baba wa Usalafiyah anasema hivi kwenye kitabu chake Iqtidaswiratal mustaqim  chapa ya  Dar Hadith ("Majma' Fatawi Ibn Taymiyya,") Mujaraba wa. 23, uk . 163:


 "fa-ta'adhwm al-Maulid wat-tikhaadhuhu mawsiman qad yaf'alahu ba'ad an-naasi wa yakunu lahu fihi ajra`adhwim lihusni qasdihi ta'adhwimihi li-Rasulillahi, swalallahu aleihi wa salaam"
"Kusheherekea  na kuitukuza  siku ya mazazi ya Kipenzi Muhammad S.A.W  na watu kufanya ni msimu wa sherehe, kama wafanyavyo baadhi ya watu  ni nzuri na wanapata ujira mkubwa katika  kutokana na nia yaonjema kwa jambo hili la kumuenzi Rasullulah swalallahu aleihi wa salaam"
Ibn Tay'miah anaendelea kwa kusema  katika kitabu chake hicho,  ukurasa wa 266 sentensi ya 5  toka chini Kwa jinsi watu wanavyofanya  wakati wa sherehe hizi za maulid  kama ni ushindani  dhidi ya wakiristo wafanyavyo wakati wa kirisimasi kusheherekea uzao wa Nabii Issa aleihisalaam au ni hali ya kuonyesha mahabba kwa kipenzi chetu Muhammad swalallahu aleihi wa salaam  na dalili ya mapenzi juu ya Mtume wetu kipenzi swalallahu aleihi wa salaam, Allah atawalipa malipo mema kwa ijtihad yao hiyo mbali ya kuwa kitendo hiki ni bida’a. Hii ni kutokana na mapenzi yao na nia yao njema kwa suala hili. Ibn Taymiah anaendelea kusema, "Twajua kuwa Maulid haikuwahi kufanywa  na salaf, wangeifanya kama wangetaka kwani hakuna kipingamizi chochote cha kisharia kilichowakataza waisifanye maulid"
Kipande hiki na vingine vingi  mno katika vitabu vya Ibn Taymiah na wengineo vimeondoshwa kwa makusudi kabisa na Masalafiyah( Mawahabi) kama wafanyavyo kwenye vitabu vingi vya Sunnah na maandiko ya kihistoria kupotosha ummah. Kuna  editor wa Kiwahabi kwa jina Muhammad Hamid al Fiqqi , ameandika maneno yafuatayo kwenye sherhe yake chini kwa mshangao mkubwa sana eti…"kayfa yakunu lahum thawabun ala hadhaa…?Ayu ijtahadun fi hadhaa??"
Ibn  Jawz ameandika kitabu cha mashairi kuhusu mazazi ya Mtume (Maulid), Ibn Jawz ameandika kitabu cha maulid kwa mashairi  kwa kuanza na beti hii….Alhamdullilah al-ladhiy abraza ghurrati aru’si al hadharat subhan Mustanira……
Na Imam Ibn Hajar al Asqalani ameandika Katika kitabu al Durar al kamina fi ayn al mi’at al thamina  anasimulia kuwa Ibn Kathir  Muhadith na pia mfuasi wa karibu mno wa Ibn Taymia ya kuwa kabla ya umauti wake Ibn Kathir aliandika kitabu kinaitwa Maulid Rasullullah. Kitabu kimeandika juu ya ruhusa ya kuwepo na kufanywa maulid  na kuonyesha kuwa hakuna ubaya kusherehekea mazazi ya Mtume swalallahu aleihi wa salaam. 
Kwa maelezo zaidi ya Bida’a3 fuatilizia mfululizo wa Video za Al Akh AlKarim Al-Habib Mbarak Ahmed youtube au kwenye viunga vya blog hii (video za kiswahili)
Wa Billah Tawfiq

2 comments:

  1. taja vitu ambazo haziukua wakati wa mtume na zipo sasa ambazo nikatika dini

    ReplyDelete