Sunday, February 12, 2012

Swali kuhusu Falaki Na Hukumu Yake...

Swali:

Je, Falaki ni nini na ni nini hukumu yake?

------------------------------------------------------------------------------------------
Jibu:

Swali haliko wazi. Ni vyema mtu akiuliza swali afafanue wazi wazi anauliza kuhusu nini khasa?

Ikiwa swali ni kuhusu Elimu ya Falaki, ambayo kwa Kiingereza ni Astronomy, pamoja na matawi yake mengine, kama vile Astrophysics (Fisikia ya Umbile za Falaki); Astrometry (Fisikia ya Mienendo na Miale ya Sayari); Cosmology (Elimu ya asili na maumbile ya Ombwe\Anga la juu) na kadhalika –mingoni mwake Elimu ya Utabiri wa hali ya hewa; ambayo ni Elimu ya maumbile ya Ulimwengu na Dunia yetu hii – Nyota, Sayari: kama Jua na Mwezi, Mbingu- inayoelezea na kuchambua maumbile ya vitu hivi, mienendo yake, tabia zake na mahusiano yake na kadhalika- basi Elimu hiyo ni halali kabisa. Bali, naweza kusema kuwa, kama zilivyo Elimu nyengine, ni Fardhi Kifaya kwa Waislamu. Yaani, iwapo patatokea kuwa hakuna mtu aliyesomea Elimu hiyo katika Jamii fulani ya Waislamu, basi Waislamu wale watakuwa wamekosea na wanaweza kupata dhambi kwa Mwenyezi Mungu, S.W.


Elimu ya Falaki – niliyoifafanua hapo ljuu- ina faida kubwa sana na umuhimu mkubwa katika kuelewa siyo tu Quráni Tukufu na Sunna za Mtume S.A.W., bali pia kuelewa na kuhisi kwa dhati Utukufu wa Mwenyezi Mungu S.W., na jinsi ya kutokuwa na mshirika yeyote katika Uungu wake na Utukufu Wake. Ni Elimu ambayo Mwenyezi Mungu S.W. amewatambia binaadamu, mara kwa mara, katika Kitabu Chake Kitukufu akiwataka waangalie na kutafakari juu ya vitu alivyoviumba na ambavyo vipo mbele ya macho yao, ili waweze kujua kuwa hakuna aliyeviumba vitu hivyo isipokuwa Yeye S.W. Kwa mfano: Mwenyezi Mungu anasema kwenye Surat Fussilat:Q.41 aya 53: Tutawaonesha alama zetu kwenye peo za mbali (horizons) na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya (wnayoelezwa) ni ya kweli. Je! Haikutoshi kwa Mula wako kuwa Yeye ni mjuzi wa kila kitu?

Ni katika elimu hii ndipo tunapojua majira ya sala; majira ya Hija; Majira ya Kufunga na kufungua; njia za usafiri katika ardhi, bahari na angani; mienendo ya miezi, mifungo miaka, miongo na karne; majira ya mvua na jua; misimu ya kupanda na misimu ya kuvuna; athari za miale ya jua; baridi na joto; udhaifu wa mwanadamu; uchache wa elimu ya mwanaadamu; Utukufu wa Mwenyezi Mungu; Hakika ya Upweke wa Mwenyezi Mungu na kadhalika.

Ni kutokana na Elimu hii, Astronomy na baadhi ya matawi yake niliyoyata hapo juu, ndiyo hawa wakubwa wa karne yetu hii waliozozitumia na kuendelea kuzitumia kuingia katika Anga za Juu na kutua katika Mwezi na kwenye Sayari nyengine, wakielewa sawasawa changamoto waliopewa na Mwenyezi Mungu S.W. katika Surat al-Rahman, ambamo Mwenyezi Mungu, S.W. anayowatambia na kuwasuta viumbe vyake: Majini na binaaadamu, kwa kusema: Enyi jamii ya majini na watu! Kama mtaweza kupenya katika mbingu na ardhi basi penyeni. Ila msipenye ila kwa kuwa na nguvu (sultan= power). Basi ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha (kuwa si neema yake)? Q.55. aya 22 na 23.

Ni katika sura hiyo hiyo ambayo ufunguzi wake pia unahusu masuala hayo hayo.. Mwenyezi Mungu anasema:

Kwa jina la Mwingi wa Kurehemu. Amefundisha Qur’ani. Amemuumba binaadamu. Akamfundisha ufafanuzi. Jua na mwezi (huenda na kuzunguka) kwa hesiabu (zake) Na nyota na miti inamnyenyekea (Mwenyezi Mungu). Na mbingu ameiinua juu na akaweka mizani (uadilifu). Ili msidhulumu katika mizani (kutoa haki). ………. Basi ipi katika neema za Mola wenu mnayoikanusha?!

Ni wazi, kwa mwenye akili timamu na mwenye kutafakari saana, kwamba Mwenyezi Mungu S. W. hakututaka sisi wanaadamu tuelewe Utukufu Wake na Ungu wake, kwa kuangalia tu Anga la Juu na uzuri wa Jua na Mwezi. La! Ametutaka tuangalie kwa makini na tujifunze na kujua vipi Anga la Juu na viliyomo ndani yake vinafanya kazi, kwani kwa kufanya hivyo ndipo tutapoweza kuelewa Utukufu Wake. Anasema katika Surat Yasin:

Na dalili kwao ni (vile) Usiku tunavyouchuna kutoka kwenye mchana: mara wanaingia gizani! Na mwezi tumeupimia vituo; mpaka unarudi na kuwa kama chaparare la mtendo kuukuu. Haiwezekani jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaelea katika mzunguko wake . Q:36.34-40.

Ni Qurani Tukufu, ambayo lau kama tungeliisoma kwa makini na kuitafakari na kuzingatia changamoto zake tungeelewa kitambo kwamba Dunia ni duara na si mfuto. Mwenyezi Mungu S.W. anasema kwenye Surat al-zumr:

Ameumba mbingu an ardhi kwa haki; huuvingirisha usiku juu ya mchana na huuvingirisha mchana juu ya usiku; na amerahisisha jua na mwezi, vyote vinatembea kwa muda ulioekewa, Jueni kwamba Yeye (Mwenyezi Mungu) pekee ndiye Mwenye Nguvu na Mwingi wa kusamehe! Q.39.5.
خلق السماوات والأرض بالحق يكور الليل على النهار ويكور النهار على الليل وسخر الشمس والقمر كل يجري لأجل مسمي ألا هو العزيز الغفار.( الزمر:5)
Yote hayo utawezaje kuyajua kama hukusoma elimu ya Falaki?!!!

Kwa ufupi, Elimu ya Falaki na matawi yake yote ni Elimu sahihi na ni muhimu sana katika kuelewa Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna za Mtume Wake na zaidi katika kuelewa Utukufu wa Mwenyezi Mungu S.W. na Upweke wake wa kutokuwa na mshirika au kuweko kitu mfano Wake!

LAKINI ikiwa kwa falaki unakusudia elimu ya UNAJIMU na UTABIRI wa mambo yatayotokea baadaye basi hiyo SI Elimu, bali ni udanganyifu na ujambazi unaofanywa na watu wakosefu wa imani. Maana kama kweli elimu hiyo ipo na kweli inaweza kubashiri kwelikeli yatayotokea baadaye, basi wenye elilmu hiyo wangeweza kutabiri wao wenyewe watakufa lini, saa ngapi na wapi, achilia mbali kuwatabiria wengine mambo yao ya baadaye. Wangeweza kuzuwiya maradhi yao wenyewe yasitokee au kuwakumba kabla ya kuzuwia maradhi ya wengine. Wangeweza kutabiri na kutupunguzia maafa mengi duniani kabla ya kutokea! Lakini wapi! Hawawezi! Ni wadanganyifu tu. Anayefanya hivyo ni mshirikina na aneye enda kwake na kuamini kwama anaweza kujua ghaibu, mambo ya baadaye, eti kwa elimu yake tu ya unajimu, basi na yeye pia ni mshirikina. Kuna aya za Qurani kem kem kuhusu jambo hilo na hadithi za mtume S.A.W. kem kem kuhusu uharamu huo.

: (قُل لا يَعْلَمُ مَن فِى السَّمَوَاتِ وَالأرْضِ الْغَيْبَ إِلا اللَّهُ وَمَا يَشـْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ) (النمل: )65.
(وَلِلَّهِ غَيْبُ السَّمَوَاتِ وَالأرْضِ وَمَآ أَمْرُ السَّاعَةِ إِلا كَلَمْحِ الْبَصَرِ أَوْ هُوَ أَقْرَبُ إِنَّ اللَّهَ عَلَى كُلِّ شىْءٍ قَدِير(ٌ{ النحل: 77. }وَعِنـْدَهُ مَفَاتِـحُ الْغَيْبِ لا يَعْلَمُهَآ إِلا هُو)َ( الأنعام: )59.
وأمر سبحانه نبيه صلوات الله وسلامه عليه أن يعلن على الملأ أنه لا يعلم الغيب: }قُل لا أمْلِكُ لِنَفْسِى نَفْعًا وَلا ضَرٌّا إِلا مَا شـَآءَ اللَّهُ وَلَوْ كُنتُ أعْلَمُ الْغَيْبَ لاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الخيْرِ وَمَا مَسَّنِى السُّوءُ إِنْ أَنـَا إِلا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِقَوْمٍ يُؤْمِنــُونَ{ الأعراف:

أوَلَمْ يَنظُرُواْ فِى مَلــَكُوتِ السَّمَوَاتِ وَالأرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّهُ مِن شَىْءٍ وَأَنْ عَسَى أن يَكُونَ قَدِ اقْتَرَبَ أَجَلــُهُمْ{ الأعراف: 185.
(أَفَلَمْ يَنـْظــُرُوآ إِلَى السَّمَآءِ فَوْقَهُمْ كَيْفَ بَنـَيْـنَاهَا وَزَيَّنــَّاهَا وَمَا لَهَا مِن فُرُوجٍ{ سورة ق: 6، }إِنَّ فِى خَلْقِ السَّمَوَاتِ وَالأرْضِ وَاخْتِلافِ اللــَّيْلِ وَالنــَّهَارِ لآيَاتٍ لأوْلِى الألْبَابِ*الـَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللــَّهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَى جُنــُوبِهِمْ وَيَتَفَـكَّرُونَ فِى خَلْقِ السَّمَوَاتِ وَالأرْضِ رَبـَّـنـَا مَا خَلَقْتَ هَذَا بَاطِلاً سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النــَّارِ{ آل عمران: 190،


Hii haina maana kwamba mtu ni haramu kutabiri kitatokea nini endapo kutaonekana wazi wazi kuweko kwa dalili inayopelekea kutokea kitu fulani. Kwa mfano, utabiri wa mvua, jua, theluji, radi na kadhalika kutokea katika maeneo fluani na katika nyakati fulani kutokana na kujua hali ya hewa na mienendo ya mawingu na upepo, na kadhalika. Kutabiri uwezekano wa mtu kuwa na maisha mafupi, pengine ya masiku kadhaa, kutokana na kuharibika kwa vitu au viungo fulani ndani ya mwili wa mgonjwa. Kutabiri kuripuka kitu fulani kwa vile kuna dalili ya kuweko kilipuzi, na kadhalika. Kutabiri jinsia ya mtoto mchanga aliyoko tumboni kwa mama yake kutokana na kuona mwili wa kichanga hicho kupitia zana za xray – kama nilivyoelezea hapo juu kuhusu elimu ya Astrometry. Utabiri kama huu, ambao Mwenyezi Mungu amewekea dalili zake na sababu zake wazi wazi, hauitwi unajimu! Bali ni utabiri wa matokeo ya kitu fulani kutokana na sababu zake ambazo ziko wazi na zimepangwa na Mwenyezi Mungu kuwa ikitokea x basi kutakuweko y, na ikikosekana y basi kutatokea z., etc., etc.

 Wa Billahi al-Tawfiq.
 Dr. A. Shareef.

No comments:

Post a Comment