Friday, February 24, 2012

Swali kuhusu Kuapa/Kula yamini...


Maswali:


Je, nini maana ya kuapia (WALLAHI !)
Je, mtu anapoapia hivyo wakati ni kitu cha uongo inakuaje?
Nini hukmu ya mtu anaeapia kwa uongo au kwa maslahi fulani ambayo ni ya uongo!
Je, yafaa kuapia kila mara?

Majibu:

Bismillahi!
Kuapa, au Kula kiapo, au Kula Yamini, katika Uislamu, kunamaanisha “kutoa dhamana kwa mtu mwengine au watu wengine, au kumthibitishia, kwa kutumia Jina la Mwenyezi Mungu au mojawapo wa Sifa Zake, kwamba jambo fulani linaloapiwa – na ambalo halina ushahidi wazi wazi- ni kweli na sahihi kama
linavyodaiwa na mwenye kula kiapo hicho na hivyo basi ni budi kusadikiwa madai hayo kwani Mdhamini Mkuu ni Mwenyezi Mungu, Mjuzi Pekee wa ukweli au uwongo wa mambo yaliyofichika nyoyoni!

Mfano wake kusema: Wallahi nasema kweli! Wallahi jambo fulani ni kweli! Wallahi mimi nimeuona mwezi umeandama! Wallahi kitu hiki ni changu! Wallahi sitofanya jambo fulani! Maana yake: Natoa dhamana na nathibitisha, Kwa jina la Mwenyezi Mungu, kwamba mimi nasema kweli, etc., etc. Hivyo basi, kiapo LAZIMA kiwe kwa mojawapo wa majina ya Mwenyezi Mungu PEKEE, au mojawapo wa Sifa zake; kama Wallahi, Billahi, Tallahai, Wa Rabil-Ka’ba, Naapa kwa Yule ambaye roho yangu iko mikononi Mwake (ukimaansha Mwenyezi Mungu). Kuapa kwa jina lolote lile, jengine, lisilokuwa la Mwenyezi Mungu, au kwa sifa yoyote ile nyengine, isyokuwa ya Mwenyezi Mungu, ni HARAMU na ni sawa na USHIRIKINA, KUFR! Mtume S.A.W. amesema:

من حلف بغير الله فقد كفر وأشرك (رواه الترمذي) Anaye apa kwa jina lisilokuwa la Mwenyezi Mungu amekufuru na kumshirikisha (Mwenyezi Mungu).

Kwa maneno mengine: Kuapa ni kutumia Jina la Mwenyezi Mungu au mojawapo wa Sifa Zake kuwa ndiyo dhamana ya ukweli wa jambo fulani au tamko fulai au ni ahadi HALALI inayotolewa na mla kiapo kwamba jambo hilo au ahadi hiyo ni kweli kabisa isiyo na mushkeli wa aina yoyote! Ni dhamana nzito na kubwa sana isiyopingika hata kidogo isipokuwa kwa yamini nyengine ya kupinga dai hilo; na kama ni kuhusu ahadi, basi ni ahadi nzito na kubwa sana ambayo haina budi kutekelezwa kama ilivyoahidiwa; venginevyo, ghadhabu na hasira za Mwenyezi Mungu, au hata laana Zake, zimshukie huyo aliyesema uwongo na kudanganya kwa kutumia Jina Lake! Zaidi, ahadi inayotolewa lazima iwe ya halali, mtu hawezi kuapa kwa kusema: Wallahi nitazini! Hapo anapata dhambi kubwa sana ka kutumia jia la Mweanyezi Mungu kuahidi kum’aswi!!!!!

Ni kutokana na uzito huo ndipo Mwenyezi Mungu S.W. amekemea kutumilia Jina lake, ovyo ovyo, na kulifanya kama chambo cha madai au ahadi za upuuzi puuzi, kwa kusema:

: وَلا تَجْعَلُوا اللَّهَ عُرْضَةً لِأَيْمَانِكُمْ [البقرة:224]، وقال تعالى: وَاحْفَظُوا أَيْمَانَكُمْ [المائدة:89]
“Na wala msimfanye jina la Mwenyezi Mungu kuwa chambo cha ulaji yamini zenu”, al-Baqara: 224. “ Na chungeni (lindeni) ulaji yamini zenu!”, al-Ma’ida: 89.

Katika surat al-Qalam, Mwenyei Mungu anamuelezea mtu apendye kula yamini ovyo ovyo na hasa katika mambo ya kipuuzi puuzi, kuwa ni mdharauliwa asiyefaa kuaminiwa:

وَلا تُطِعْ كُلَّ حَلَّافٍ مَهِينٍ [القلم:10]
“ Na usimsikilize (usimkubalie\usimuamini) kila mwingi wa kuapa mdharauliwa” Na Anamuelezea mtu wa aina hiyo, katika aya zinazofuatia kuwa ni “ Mtapitapi, apitaye akifitini, mwenye kuzuia kheri, dhalimu, mwingi wa madhambi” al-Qalam: 11-12.

Kutokana na utangulizi huo, tunaweza kujionea wenyewe siyo tu uzito wa kula yamini au kuapa kwa kutumia Jina la Mweyezi Mungu na ubaya wa kuapa ovyo ovyo, lakini pia ubaya wa kulitumia jina la Mwenyezi Mungu katika mambo ya upuuzi puuzi, mazungumzo ya kawaida yasiyohitaji kuapiwa au kuliwa yamini.

Aina za viapo:

Kuna viapo vya aina tatu katika Uwislamu- yaani Kisheria.

1). Kwanza , لغو اليمينkiapo kisichokusudiwa. Hiki ni kile kiapo kinachomtoka mtu katika mazungumzo ya kawaida tu¸pasipokuwa na maana ya kutoa dhamana au ahadi, au hata ithibati yoyote, kuhusu analolizungumzia, bali ni kuapa kama pambo tu la mazungumzo. Kwa mfano, mtu katika mazungumzo yake ya kawaida, kusema: “ Wallahi nasikia njaa!”; “Wallahi jana niliota ndoto mbaya!”, au mtu unamuuliza: Fulani yuko? Anakujibu: Wallahi hayupo! etc. etc.

Hukumu yake, SI vizuri mtu kuapa-apa bila ya sababu au kugeuza jina la Mwenyezi Mungu kuwa pambo la mazungumzo tu! Ikiwa anafanya hivyo, kwa makusudi, basi anakua anadharau Jina la Mwenyezi Mungu, na hapan shaka Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye atampatiliza vipi. Lakini ikiwa ana-apa bila ya dharau au bila ya kusudio la kuthibitisha au kukana jambo analolizungumzia, bali ni pambo tu la mazungumzo, basi ni makruh= yaani si vizuri kufanya hivyo. Yaani ni tabia isyopendeza katika Uwislamu! Hii inaitwa Laghwi-alyamin= yamini puuzi. Hakuna dhambi, wala kafara; kwani aliyeapa ametumia jina la Mwenyezi Mungu kama pambo tu. Mwenyezi Mungu anasema:

: لَا يُؤَاخِذُكُمُ اللَّهُ بِاللَّغْوِ فِي أَيْمَانِكُمْ [البقرة:225]
“ Mwenyezi Mungu hakupatilizeni katika yamini zenu puuzi”.

2). Yamini ya pili ni ile inayoitwa: Yamin al-Ghumuus Yamini ya uwongo! Hii ni yamini anayekula mtu, akijuwa wazi wazi kuwa anayoyasema ni uwongo, lakini anatumilia Jina la Mwenyezi Mungu kudanganya, kudhulumu, kwiba, kughushi na kadhalika. Mfano mtu kusema: Wallahi nyumba hii niliinunua kutoka kwa Marehemu fulani (kumbe ni uwongo!) Wallahi fulani amenifanyia dhululma fulani! (kumbe uwongo, anakula yamini ili ajipatie manufaa) Wallahi mimi ni mtoto wa fulani!, etc., etc. [Kinyume ya Yamin al-Ghumuus ni Yamin ya Ukweli –ambayo ni Ithbati au Ushahidi wa jambo la kweli. Yamini ya Ukweli, ni halali na inaweza kuwa Wajib, yaani ni Lazima mtu ale yamini hiyo, iwapo ushahidi wake katika jambo la kweli unahitajika. Kwa mfano: Wallahi nimeuona mwezi wa kuandama mfungo wa Ramadhani! Hapa ni wajibu kuthibitisha kuonekana kwa mwezi andama, ili Waislamu wafunge! Yamini ya Ukweli ina thawabu na Yamini ya Uwongo ina dhabi kubwa sana]

Yamini ya Uwongo ni dhambi kubwa sana, na mojawapo wa madhambi makubwa katika Dini, dhambi ambayo, hata kafara haiwezi kuifidia na kufuta dhami zake, haina kafara hata kidogo, na mwenye kula yamini ya uwongo basi anatoka katika Uwislamu na akifa bila ya kutubu anakufa akiwa SI mwislamu – wal’iyadh Billah! Mtume S.A.W. amesema:

الكبائر: الإشراك بالله وعقوق الوالدين وقتل النفس واليمين الغموس

“ Madhambi Makubwa ni: Kumshirikisha Mwenyezi Mungu; Kutotii wazee wawili; Kuua Nafsi (bila ya haqqi) na Yamini ya uwongo”. Bukhari.

Hadithi nyengine, bedui mmoja alimwendea Mtume S.A.W. akamuuliza: Madhambi makubwa kuliko yote ni yepui? Mtume S.A.W. akajibu: Kumshirikisha Mwenyezi Mungu! Bedui aksema: Nini jengine? Mtume akasema: Yamini ya Uwongo (al-Yamin al-Ghumus)! Sahaba mmoja akauliza; “Ndiyo nini Yamin al-Ghumus?”.. Mtume akasema: “ Yamini ya kupora mali ya Mwislamu mwengine”. Bukhari.

3). Yamini halali kisheria, ambayo mtu anaapa, kama ahadi, kwamba atafanya\au hatofanya jambo fulani, ambalo ni halali, au anaapa kuthibitisha jambo fulani mbele ya watu wengine, etc. etc. Kwa mfano: Wallahi sitatembelea nchi fulani maisha yangu yote! Wallahi nitaenda Umra mwezi ujao! Wallahi nitamuoa\nitaolewa na fulani mwakani!, etc etc. Yamini kama hii ni halali na aliyekula yamini hiyo hana budi kutekeleza ahadi yake kama alivyoitoa. Endapo akija kubadilisha ahadi yake, au akaona kuwa kufanya aliloahidi kutolifaya ni bora zaidi kuliko kuendelea na ususaji wake wa jambo hilo, basi anaruhusiwa kwenda kinyume na ahadi yake hiyo; yaani KUJIKOMBOA katika kifungo alichojiingiza kwa yamini, kwa kutoa kafara (kutoa FIDIA) ya yamini yake, endapo atavunja ahadi hiyo. Na kafara ni kama ilivyotajwa katika Qur’ani, Surat al-Ma’ida aya ya 89, isemayo:

“ Mwenyezi Mungu hatakupatilizeni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atakulipatilizeni kwa mnavyo apa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnacho walisha ahali zenu, au kuiwavisha, au kumkomboa mtumwa. Asiye pata hayo, basi afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapo apa. Na chungeni yamini zeyu. Nanma hivyo Mwenyezi Mungu anakubainishie ni Aya zake ili mpate kushukuru”.

Yaani kafara ya yamini ni kwa mpangilio ufuatao:

i).Kulisha masikini kumi chakula cha wastani unacholisha familia yako, au
ii).Kuwavisha nguo masikini kumi, au
iii).Kumkomboa mtumwa. Yaaani ni khiyari ya kufanya moja kati ya hayo mambo matatu. Iwapo bado mtu hamudu lolote katika mambo hayo matatu, basi
iv).afunge siku tatu – sawmu ya kafara ya yamini.

Mtume S.A.W. anatubainishia sababu ya kuvunja ahadi ya yamini na pia wakati gani kafara hiyo inatolewa, aliposema:

من حلف علي يمين فرأي غيرها خيرا منها فاليكفر عن يمينه وليفعل الذي هو خير ( رواه مسلم )
“Aliyekula kiapo kufanya jambo, akaona kufanya venginevo ni bora zaidi basi atoe kafara ya yamini yake na atende hilo liliokuwa bora” Muslim.

Yaani kwanza atoe kafara kisha atende hilo ambalo ni bora zaidi kulifanya kuliko lile aliloahidi kulifanya au kutolifanya. Endapo atavunja ahadi yake ya yamini au akabadilisha maoni yake na akatenda lile ambalo aliahidi kutolitenda, na papo asitoe kafara au fidia basi anaingia katika mkumbo wa Yamini ya Uwongo!

Natumai kuwa maelezo hayo, machache, yanajibu maswali yaliyoulizwa na ukht Fatma, na pia kufafanua umuhimu na uzito wa yamini, na hasa onyo la kujiepusha kula yamini ovyo ovyo katika mambo ya upuuzi, kwani kufanya hivyo kunaweza kupelekea kuwa ni kudhalilisha na kudharamu Jina la Mwenyezi Mungu. Zaidi mtu akijulikana kuwa anapenda kuapa-apa katika kila jambo, dogo na kubwa, muhimu na lisilomuhimu, basi anaweza kuhesabika kuwa ni Mwongo, Mnafiki na kadhalika. Ni vyema, kuchukua tahadhari kubwa katika kula yamini au kuapa; ikiwa pamoja na kujiepusha kuapa kwa majina yasiyokuwa ya Mwenyezi Mungu.

Swali la nyongeza...
Je, kuapa kwa kusema "Haki ya Mungu na Mtume" au nimesikia "Mashaf ya Mtume" au Wallahi wa Rasuli" ni katika haramu?.

Jibu:

Hadithi ya Mtume S.A.W. isemayo kuwa ni haramu kuapa kwa jina la kiumbe yeyote yule, au kwa jina lolote lile isipokuwa jina la Mwenyezi Mungu inatoa jibu kuhusu maswali uliyouliza! Yaani ni haramu! kwa maana hiyo, hiyo, Msahafu SI jina la Mwenyezi Mungu, bali ni Kitabui cha Mwenyezi Mungu, ambacho ni sahihi kuugusa Msahafu wakati wa kuapa kwa Jina la Mwenyezi Mungu, lakini si kwa msahafu wenyewe. Kuna tofauti baina ya Msahafu- na Qur'ani au Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Msahafu ni buku la maandishi juu ya karatasi ya aya za Qur'ani. Karatasi na gamba lake ni vitu tunavyotengeneza sisi wanaadamu. Lakini ni tofauti na mabuku au vitabu vengine; maana kitabu hicho kina maandishi ya maneno ya Mwenyezi Mungu. Hivyo, msahafu SI jina la Mwenyezi Mungu wala si mojawapo wa sifa Zake. Lakini maandishi yaliyomo ndani yake ni alama za kutuwezesha sisi kuandika maneno ya Mwenyezi Mungu na kwa maana hiyo yale yaliyomo ndani yake, ka ujumla wake, ni Maneno ya Mwenyezi Mungu, ambayo kwa ujumla wake tunaita Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Kwa ajili hiyo, ndiyo tunakitukuza Kitabu hicho na tunafika hadi kuwa hatupendi kukigusa bila ya kuwa na tohara. Kwa sababu ni buku au kitabu chenye alama za maneno ya Mweanyezi mungu, basi tunakigusa wakati wa kula kiapo- siyo kama ni jambo la lazima, la- bali ni kutilia mkazo kiapo chetu tu.

Majina ya kuapia yanasalia kuwa ni majina ya Mwenyezi Mungo pekee na si majina au kitu au mtu mwengine yeyote yule. Ama kuhusu swali lako la Haki ya Mungu na kadhalika - matamshi ambayo yanatumika sana upade wa Tanzania Bara, naamini hiyo ni sehemu ya Laghw al-Yamin, matumizi ya lugha zaidi kuliko ikuwa Kiao cha Kiislamu! Hata utumizi wa kiapo hicho, mara nyingi huwa katika mazungumzo ya kawaida tu na SI kwamba ni sehemu ya Kiapo cha Kiislalmu.

Ni vizuri mtu kuepuka kutumia maneno hayo, maana Haki ya Mungu ninavyo elewa na kufahamu mimi ni kuwa kila kitu kilichomo duniani na kwengineko ni vitu vya Mwenyezi mungu. Sasa iweje tuape kwa vitu hivyo?!!!! Ilimradi si elewe kikamilifu nini hasa kusudio lake. Mingi ningejaribu kuepuka kutumia maneno hayo ikiwa ni sehemu ya kujiepusha na mambo ya SHUBHA au Yamini za upuuzi!

Je, vipi kuhusu viapo vilivyo ndani ya Qur'an...kama vile "Wa teeni wa Zaytooni..." n.k?

Ama kuhusu viapo vilivyomo ndani ya Qur'ani, hivyo ni Viapo vya Mwenyhezi Mungu MWENYEWE, ambavyo SISI wanaadamu hatuwezi kuvitumia kuapia. Mwenyezi Mungu anaapa kwa vuti mbali mbali alivyoviumba na ambavyo ni mojawapo wa dalili za Uungu Wake na Utukufu Wake. Wateen wa al-Zaytun, wa Turi siineen, Wa hadha al-baladi al-Amina: Yaani Naapa kwa tunda la Tini na Zaytuni, na Jabalo la Turi Sineed, na Huu mji Mtulivu (Makka): Hakika tumemuumba binadamu katika umbo lenye mpangilio mzuri kabisa.

Hali kadhalika, anaapa kwa Jua na Mwezi, anaapa Qalamu aliyoiumba, na kadhalika, na anaapa kwa baadhi ya herufi, ama peke yake au zilizounganishwa na herufi nyengine, kama Alif Lam Meem; Kaf, Ha, Ya, 'Ain, Saad; Yasin, etc.,etc., herufi ambazo hakuna ajuaye maana yake wal malengo yake - hadi hii leo, tumepigwa na butwaa. Vyote hivyo, anatumia Mwenyezi Mungu kuapia katika kutufunza jambo au kutusimbulia jambo; maana vyote hivyo ni maumbile yake. Mwenyezi Mungu anaapa hata kwa baadhi ya majina ya Qur'ani; kwa mfano Yaseen wa al-Qur'ani al-hakeem; anaapa kwa baadhi ya Majina yake Mwenyewe, kama al-Rahmaan, etc., etc.

Kiapo cha vitu hivyo, au majina hayo ni kiapo cha Mwenyezi mungu peke yake,hana mshirika Wake katika hilo. Hivyo, kwa binaadamu, ni haramu kuapa kwa majina yoyote yale, ikiwa pamoja na majina ya matunda, majina ya siku au miaka na mifungo. Ni haramu kwetu sisi! Nakumbusha tena kuwa Mtume S.A.W. amesema: Anayeapa aape kwa jina la Mwenyezi Mungu pekee au aache kuapa!

Wa Bilah al-Tawfiq
Dr. A. Shareef.

No comments:

Post a Comment