Friday, February 3, 2012

Swali kuhusu ndoa ya Mut'ah

Swali:

Je, ndoa ya Mutta inafaa?, naomba maelezo ya ziada.

-----------------------------------------------------------------------------------------------

Jibu:

Naamini unakusudia Ndoa ya Mut’a na si Mutta. Kama ni hivyo, basi ni vyema kuitolea ufafanuzi unaostahili ili ijulakne timbuko lake, sababu zake na msimamo sahihi wa Sharia juu yake.

Neno “Mut’a”, katika lugha ya Kiarabu, linamaanisha : starehe ya muda; Kwa hivyo, “Nikah al-mut’a”
maana yake ndoa ya muda, au kwa Kiingereza: Temporary marriage. Ndoa ya aina hiyo, na ndoa nyingi nyengine, zilikuwepo kabla ya kuja Uwislamu, miongoni mwake ni ile ndoa ya mtoto kumuoa mjane wa baba yake mzazi; yaani kumuoa mama yake (!)., au kuoa wanawake ambao ni ndugu halisa, wakati mmoja. Hivyo, ndoa ya Mut’a ilikuwa ni mojawapo wa ndoa zinazotambuliwa, kabla ya Uwislamu. Na kwa vile ni ndoa ya muda, inayotajwa muda wake, basi huwa hakuna talaka. Muda ule uliotajwa ukimalizika basi ndoa yenyewe inatenguka. Hakuna ndoa tena, na kila mmoja anashika njia yake!

Ulipokuja Uwislamu, ulifutilia mbali, karibu ndoa zote ambazo haziendani na maadili na malengo ya Kiislamu; na kusaliza, kwa muda, ndoa nyengine, na baadaye kufuta moja kwa moja ndoa hizo pia. Miongoni mwa ndoa za kijahiliyya zilizoachwa kuendelea kwa muda ni ndoa ya Mut’a. Zile ambazo zilifutwa na kupigwa marufuku moja kwa moja ni pamoja na ndoa ya mtoto kumrithi mjane wa baba yake.

Q.4:22 “inasema: “Na wala msiwaoe wake walio-olewa na baba zenu, isipokuwa yale yaliyokwisha pita. Bila ya shaka jambo hili ni uovu na uchukizo na ni njia mbaya”.

Nyengine ziliyopigwa marufuku ni aina nne :-

1. Nikah al-shighaar, ambayo ni wanaume wawili kubadilishana watoto wao wa kike, kama ndoa: huyou anamuozesha mtu wa pili mtoto wake wa kike, ili na huyo aliyeozeshwa na yeye amuozeshe mtoto wake yeye, na huko kubadilishana ndio mahari (!). Ni haramu! Ibn Umar anasema: Ametukataza Mtume S.A.W. ndoa ya shighaar. Na shighaar ni mtu kumuozesha binti yake mtu mwengine kwa sharti kwamba mtu huyo naye amuozeshe yeye binti yake, na hakuna mahari baina yao”. (Imam Bukhari na Muslim: Bab Nikah al-Shighar).

2. Ndoa ya mtu kuchumbia\kuposa mwanamke ambaye ndugu yake mwenyewe amekwisha chumbia\posa. Haramu! Ila pale ndugu huyo atapofuta uchumba\posa yake. Hapo inajuzu kwa ndugu yake kuchumbia au kuposa mwanamke huyo huyo. Mtume S.A.W. amesema: “ Mwenye kuamini ni ndugu wa mwenye kuamini mwengine; hivyo si halali kwa mu’umini mmoja “kumpokonya” bidhaa mu’umini mwengine kwa kutoa bei kubwa zaidi au “kuposa” mwanamke aliyekwisha poswa na mu’umini mwengine, ila kama ataachiaa mwenyewe” (Imam Muslim)

3. Ndoa ya “mhalalishi”, yaani mtu kumuoa mwanamke aliyeachwa talaka nne kwa lengo la kumhalalishia mume wa mwanzo, aliyeacha talaka nne, aweze kumrudia mke huyo. “Mhahalishaji” anamuoa mwanamke huyo, kwa kufuata sharia zote za ndoa, na anakutana naye kimwili, na anamuacha ili aweze kurudiwa na yule wa mwanzo aliyeacha talaka nne. Yaani amemuoa kwa lengo la kumhalalishia mume wa awali aliyepigwa marufuku kumrudia mkewe, hadi baada ya kuolewa na mtu mwengine na kuachwa, kwa nja za kawaida. Ni HARAMU! Mtume S.A.W. amesema: Mwenyezi Mungu amlaani mhalalishaji na mhalalishiwaji! (Imam al-Tirmidhi). Na huo ndio msimamo wa maulamaa wengi. [baadhi ya maulama’, wachache, hata hivyo, wanonelea kuwa ndoa kama hiyo inasihi lakini wanaofanya hivyo wanapata dhambi nyingi sana; kwani wamealaaniwa na Mtume S.A.W.). Binafsi naamini msimamo wa maulamaa wengi ndio sahihi; kwani mambo ni kwa niya, na niya ya aliyeoa si kuoa yeye bali ni kumhalalishia mwengine. Haramu! Ila: Mwenyezi Mungu anajua zaidi.

4. Ndoa ya Mut’a, ambayo maana yake nimeshaitolea utangulizi hapo juu, na pia kusema kwamba huwa haina talaka. Muda wake ukiisha, aghalabu ulikuwa ni siku 3, na pengine miezi 3, etc., etc. Muda huo ukiisha tu basi na ndoa yenyewe inakuwa imekwisha, haipo tena. Ajwar!

Hukumu ya Mut’a.

Kama nilivyosema hapo awali, ndoa ya Mut’a ilikuweko kabla ya Uwislamu. Ulipokuja Uwislamu, haukufuta moja kwa moja ndoa hii. Uliiacha kwa muda iendelee, na hasa baada ya wanaume wengi wa Kiislamu kuwa wako mbali na familia zao kwa muda mrefu wakati wa vita vya jihad. Sababu nyengine kubwa ya kuiacha ndoa hiyo iendelee ni ukweli wa kwamba wanaume wengi waliuawa wakati wa vita vya jihadi, hata katika wakati wa uhai wa Mtume S.A.W. mwenyewe. Wanawake wengi sana waliachwa wajane, wengine na watoto mayatima na wanawari wengi wakakosa waume wa kuwaoa. Hali ikaanza kuwa tete. Hivyo, siyo tu ndoa ya Mut’a iliachwa iendelee, bali Mtume S.A.W. aliiruhusu, wazi wazi, maswahaba waliokuwa wako mbali na familia zao kwa muda mrefu, kuoa kwa muda huko waliko.

Abdullah Ibn Mas’ud anasema: “Tulikuwa tukipigana vita pamoja na Mtume S.A.W. bila ya kufuatana na wake zetu. Tukasema wenyewe kwa wenyewe, kwanini hatujihasi (kufunga uume, ili balaa la kuwa na matamanio liondoke na tulenge juhudi zatu katika ibada na jihad)? Mtume S.A.W. akatukataza kufanya hivyo. Baadaye akaturuhusu kuoa mwanamke kwa muda tu, ambapo tukitoa nguo kuwa ndiyo mahari.” (Imam Bukhari na Muslim).

Baadaye, hata hivyo, ndoa ya Mut’a nayo ikapigwa marufuku moja kwa moja. Hili halina hitilafu hata kidogo miongoni mwa wafuasi wa madhehebu ya Sunni. Kama iko hitilafu, baina yao, basi ni kuhusu wakati gani tu ndoa hiyo ilipigwa marufuku. Pia wanakubaliana kuwa ilipigwa marufuku wakati wa uhai wa Mtume S.A.W, na aliyepiga umarufuku huo ni yeye mwenyewe Mtume S.A.W., kama tutavyo ona hapo chini.

(Ndugu zetu wa madhehebu ya Shi’a, hata hivyo, wao wanaamini kuwa ndoa ya Mut’a ni halali na wanaiendeleza hadi hii leo, wakinukuu hadithi zao zinazoishia kwa Maimamu wau, miongoni mwao ni Sayyidina Ali bin Abi Talib.)
Hivyo basi, kuna hadithi nyingi zinazoashiria wazi wazi kuwa ndio hiyo ilikuwa ikiruhusiwa awali, lakini baadaye ikapigwa marufuku moja kwa moja. Miongoni mwa Hadithi ni hadithi hizi zifuatazo:-

a) Hadithi ya Jabir bin Abdullah ikisema: “Tulikuwa tukioa kwa muda kwa kutoa mahari tende au unga wa ngano kiasi cha mteko wa viganja viwili tu vya mkono. Tuliendelea na mtindo mwenendo huo katika uhai wa Mtume S.A.W na uhai wa (Khalifa) Abu Bakr al-Siddiq, mpaka alipokuja (Khalifa) Umar akatukataza ndoa ya aina hiyo, kutokana na tukio la Amr bin Huwairith”. (Imam Muslim) .

b) Hadith ya Sayyidina Ali bin Abi Talib (Khalifa wa 4 ). Amesema sayyidina Ali R.A.A.: “Mtume S.A.W. amekataza kuoa wanawake ndoa ya Mut’a wakati wa vita vya Khaybar (nje kidogo ya Madina); na kula nyama ya punda wa kufuga (yaani punda wa kawaida. - kinyume na punda milia). [Ndugu zetu wa Kishia, hata hivyo, hawaikubali hadithi hii, pamoja na kwamba imepokelewa kutoka kwa Sayyidina Ali bin Abi Talib (!).]

c) Hadithi ya Sabra al-Juhany aliyesema kwamba alikuwa na Mtume S.A.W. akamsikia anasema: “Enyi Watu! Hakika niliwahi kukuruhusuni kuoa wanawake kwa muda, lakini Mwenyezi Mungu amepiga marufuku ndoa hiyo milele hadi siku ya Qiyama. Hivyo basi, kama kuna mtu mwenye mwanamke aliyempata kwa njia hiyo, amwache ende zake, na wala msitake kurudishiwa chochote mlichokitoa kuwapa!”. (Imam Muslim).

Ziko hadithi nyengine vile vile zinazoelezea hali hiyo ya kuwa iliiruhusiwa awali, lakini baadaye ikapigwa marufuku milele. Hizo tulizozitaja hapa, hata hivyo, zinatosha.

Pia maulamaa wengi wanona kuwa Surat al-Mu’minun, kuanzia aya ya pili hadi aya ya 7, inaonesha kuwa ndoa ya Mut’a si miongoni mwa ndoa halali zinazoruhusiwa katika Uwislamu. Aya hizo zinasema hivi:

( قد أفلح المؤمنون ( 1 ) الذين هم في صلاتهم خاشعون ( 2 ) والذين هم عن اللغو معرضون ( 3 ) والذين هم للزكاة فاعلون ( 4 ) والذين هم لفروجهم حافظون ( 5 ) إلا على أزواجهم أو ما ملكت أيمانهم فإنهم غير ملومين ( 6 ) فمن ابتغى وراء ذلك فأولئك هم العادون ( 7

“Hakika wamefuzu Walioamini. Ambao katika Sala zao huwa wanyenyekevu. Na ambao hujiepusha na mamo ya upuuzi. Na ambao Zaka wanaitekeleza. Na ambao tupu zao wanazilinda. Isipokuwa kwa wake zao au kwa wanawake ambao inawamiliki mikono ya yao ya kuume (yaani Suria). Basi hao ndio wasiolaumiwa. Lakini anayetaka isiyokuwa hawa (wake zao na masuria wao) basi ndio wavukao mipaka (ya Mwenyezi Mungu)”. Q.24:2-7.

Wanasema Mut’a si ndoa, na zaidi lau kama ingelikuwa ndoa halali basi aya isingelisema kwamba waliofaulu ni wale tu wanalinda tupu zao isipokuwa kwa wake zao au kwa masuriya wao. Na yeyote anayetaka nje ya hawa basi huyo ni mtu aliyevuka mipaka ya Mwenyezi Mungu. Hivyo, mwanamke wa mut’a si mke wala si suriya wa ndoa. Hivyo, ni haramu maana anayetaka mwanamke kwa njia nyengine huyo ni mtu aliyevuka mipaka ya Mwenyezi Mungu.

Pamoja na hayo yote, hata hivyo, bado wapo watu wachache sana, ndani ya madhehebu ya Sunni, ambao NAO wanasema kuwa ndoa ya Mut’a inajuzu iwapo patatokea dharura au haja ya kufanya hivyo. Kwa maana hiyo, wanasema kuwa ndoa ya Mut’a haijapigwa marufuku milele. Dalili yao kubwa wanayoitumia ni aya ya Qurani, kutoka Surat al-Nisa’, ambayo wanaifasiri kuwiana na maoni yao. Aya hiyo inayosema:

:(( وَالْمُحْصَنَاتُ مِنَ النِّسَاءِ إِلَّا مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ كِتَابَ اللَّهِ عَلَيْكُمْ وَأُحِلَّ لَكُمْ مَا وَرَاءَ ذَلِكُمْ أَنْ تَبْتَغُوا بِأَمْوَالِكُمْ مُحْصِنِينَ غَيْرَ مُسَافِحِينَ فَمَا اسْتَمْتَعْتُمْ بِهِ مِنْهُنَّ فَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ فَرِيضَةً وَلا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ فِيمَا تَرَاضَيْتُمْ بِهِ مِنْ بَعْدِ الْفَرِيضَةِ إِنَّ اللَّهَ كَانَ عَلِيمًا حَكِيمًا ))[النساء:24]

“Na pia (mmekatazwa kuwaoa) wanawake wenye waume zao, isipokuwa wale iliyomiliki mikono yenu ya kuume. Hiyo ndiyo Sharia ya Mwenyezi Mungu juu yenu. Na mnahalalishiwa (kuoa wanawake) wasiokuwa hawa, muwatafute kwa mali zenu, kwa kuwaoa bila ya kufanya zina. Basi wale mnaowaoa miongoni mwao, wapeni ujira wa mahari yao uliokubaliwa. Na wala si vibaya kwenu kutoa kile mlichoridhiana, baada ya kutajwa. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye Hekima”. Q.4:24.

Wanadai kuwa aya inasema; :” فَمَا اسْتَمْتَعْتُمْ بِهِ مِنْهُنَّ فَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ فَرِيضَةً ... yaani “Na wale mnaowaoa kwa muda [ndoa ya mut’a], basi wapeni ujira uliotajwa. Na wala si vibaya kwenu kutoa mlichoridhiana baada ya kukitaja”.

Ni wazi kuwa tafsiri hiyo si sahihi, hasa kwa vile kukna hadithi nyingi ambazo zinabainisha wazi wazi kuwa ndoa ya Mut’a imepigwa marufuku, tena katika siku za mwisho mwisho za uhai wa Mtume S.A.W. Dai la kwamba ndoa za Mut’a ziliendelea tokea wakati wa uhai wa Mtume S.A.W na enzi za Abu Bakr al-Siddiq na kipindi kifupi cha uhai wa Umar bin Khattab, mpaka pale alipopiga marufuku moja kwa moja, kuwa eti ni dalili kuwa Mut’a ni halali ni dalili dhaifu sana haina msingi. Yumkini sana, kuwa ama wengine hawakupata habari za kupigwa marufuku ndoa hiyo wakati wa mtume, na katika enzi ya Umar, baada ya kuletewa kesi ya mtu aliyeoa kwa Mut’a , akatangaza hadharani kuwa ndoa ya Mut’a ni haramu na akisikia au akiletewa mtu yeyote yule ambaye amefunga ndoa ya mut’a basi atamtia adavu ya kukzini, ni dalili tosha kuwa ndoa ya Mut’a ni haramu, na imeharamishwa na Mtume S.A.W kabla ya kufa, na maswahaba wengi walikuwa wakijua hayo.

Kwa ufupi, ndoa ya Mut’a ni haramu. Haisihi.

Wa billahi al-Tawfiq

Dr. A. Shareef

No comments:

Post a Comment