Swali:
Je, kama namdai mtu na akafariki nikamsamehe, baada ya siku chache ndugu zake wakanifata na kuniambia ndugu yao aliacha usia wanilipe deni langu na nikakataa wananilazimisha, Je hapo nifanyeje?
Jibu:
Kama ulimsame deni lako alipokuwa hai kumegeuza deni hilo kuwa sadaka. Umepata thawabu. Watoto wa marehemu walipogundua kuwa kuna deni, bila ya kujuwa kuwa ulishamsamehe baba yao tokea akiwa hai,
walikuwa na niya na hima ya kumkomboa baba yao huko aliko kutokana na mali yake mwenyewe au kutokana na mali yao. Wamepata thawabu. Wamekuletea fedha hizo, na wewe ukawaaambia kuwa ulishamsamehe, lakini wao hawakuridika; au bado wanataka kujihakikishia kuwa wamemkomboa baba yao na jukumu la deni. Kwa maana nyengine, pande zote mbili zinamtakia marehemu mambo mema.
Sasa, wewe una khiyari ya kuzichukua ukazitoa sadaka kwa jina la marehemu, maana pesa hizo sasa siyo zako, au kuwaambia warithi wa marehemu wazitoe sadaka kwa jina la marehemu maana wewe umeshamsamehe tokea akiwa hai. Kwa njia zote hizo, nyote mnapata thawabu, ikiwa pamoja na marehemu.
Kama unamdai mtu na huyo unayemdai akafariki ukaamua kumsamehe deni, inakuwaje?
Jibu ni hilo hilo moja; baada ya kusamehe bado una thawabu, hasa baada ya kufa kwake; maana umemuondolea shida nyengine huko Akhera; na iwapo watoto wake wataamua kukurudishia -licha ya kuwaambia kuwa umemsamehe- basi zipokee hizo pesa na zitolee sadaka. Ukizichukua wewe ni sawa kurudia matapishi yako. Ukimtolea sadaka, sasa ni wazi unarudufisha thawabu zako:
1). thawabu za kumpunguzia shida alipokuwa hai kwa kumpa mkopo;
2). thawabu za kugeuza deni hilo kuwa sadaka yako baada ya yeye kufariki, au thawabu za kumkomboa huko aliko; na
3). thawabu za kumtolea sadaka.
Thawabu juu ya thawabu!
Wa billah al-Tawfiq
Dr. A. Shareef
No comments:
Post a Comment