Kutokana na kuulizwa suala hili la “ Uganga”, “ Unajimu”, “ Utabiri”, “ Ukahini”, “ Uchawi”, “ Urogaji”, “Ramli”, “Piga bao”, na kadhalika, na ubabaishaji unatolewa na baadhi ya watu kuhalalisha au kusema si haramu, inajuzu katika Uislamu na kadhalika, nimeona niongozee hapa baadhi tu ya hadithi za Mtume S.A.W. ambazo zimepokelewa na Maimamu mbali mbali katika vitabu vyao vya Hadithi na kuekewa fafanuzi mbali mbali kwamba yote hayo ni HARAMU na ni mambo yasiyokubaliwa katika Uwislamu; na kwamba majina yoyote yatayotumika au kutumiliwa katika nyanja hizo hayawezi na wala hayataweza kuhalalisha vitendo hivyo.
Wale wanaofanya vitendo hivyo ni wadanganyifu, mabazazi, matapeli, malaghai, majambazi, walowezi kama zinavyo elezea hadithi hizi hapa chini na nyingi nyengine. Na wale ambao wanawaendea au kuwaamini katiak udanganyifu wao na utabiri wao basi na wao wamo chungu kimoja na wdanganyifu huo kama zinavyoelezea hadithi hizo.
Atakeye pendelea kuendelea na amali hizo aendelee tu lakini kuendelea kwao huko hakuwezi kufuta mafnzo ya Mtume S.A.W. wala kukadhibisha quli hizo. Mwenyezi Mungu atustiri na atulinde na kumkufuru na kumshirikisha katika Ungu Wake S.W.
Hizi hapa hadithi zenyewe na tafsiri yake:
عن صفية بنت أبي عبيد عن بعض أزواج النبي صلي الله عليه وسلم قال صلي الله عليه وسلم: من أتي عرافا فسأله
عن شيئ فصدقه لم تقبل له صلاة أربعين يوما (روا مسلم)
Amesema Safiyya kutoka kwa baadhi ya wakeze Mtume S.A.W. kwamba amesema Mtume S.A.W.: “ Mwenye kumuendea mtabiri (mpiga ramli, mnajimu, mganga, etc., etc.) akamuuliza jambo na akasadiki, hatokubaliwa swala yake kwa muda wa siku 40. (Imepokewa na Musllim)
[Amesema Imam al-Mundhiri na Imam al-Nawawi na maulamaa wengi sana kuwa: ARRAF ni mtu anayejidai kuwa anajua kutabiri mambo kutokana na hisabu maalum au viashirio fulani na hivyo kujua yatayotokea baadaye. Majina mengine yanayotumiwa ni Kahini (mganga) munajjimu (mnajimu au mtabiri) na pia mchawi. (al-Targhib wa al-Tarhib p.525) yaani majina yote hayo ni majina ya yanayofanana sawasawa]
Zinduko: Ikiwa mwenye kumuendea tu na kusadiki hukumu yake ndiyo hiyo, je yule aliye-endewa na kujidai utabiri huo yuko hali gani, mbele ya Mwenyezi Mungu?!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!!
Hadithi ya Pili.
عن عمران بن حصين قال رسول الله صلي الله عليه وسلم: ليس منا من تطير أو تطير له أو تكهن أو تكهن له أو سحر أو سحر له ومن أتي كاهنا فصدقه بما يقول فقد كفر بما أنزل علي محمد ( رواه البزار والطبراني)
Amesema Imran bin Husay R.A. amesema Mtume S.A.W.: “ Hawi mmoja wetu (si miongoni mwetu) mwenye kujikorofisha au kukorofishiwa, au mwenye kuganga au kugangiwa (piga ramli au kupigiwa ramli, tabiri au tabiriwa) mwenye kuroga au kurogewa . Na mwenye kumuendea mpiga ramli (mtabiri, mnajimu) na akamuamini anayomuambia basi amekanya (amekufuru) aliyoteremshiwa Muhammad S.A.W.
NB. Sehemu ya mwisho ya Hadithi hii isemayo: “Mwenye kumuendea mganga (mpiga ramli, mnajimu, mtabiri) na akamsadiki anayomwambia basi amekufuru aliyoteremshiwa Muhammad S.A.W.” imepokewa pia na Maimamu wafuatayo: Abu Daud hadithi nambari 3904; Timrmidhi, hadithi nambari 135; Nasa’i, hadithi nambari 9017, Ibn Majah, hadithi nambari 639; na al-Hakim hadithi nambari 8.
Hadithi ya tatu.
عن إبن مسعود رضي الله عنه قال " من تي عرافا أو ساحرا أو كاهنا فسأله فصدقه بما يقول فقد كفر بما أنزل علي محمد صلي الله عليه وسلم
Amesema Ibn Mas’ud R.A. “ Mwenye kumuendea mtabiri, au mchawi au mpiga ramli na akamsadiki anayomuambia basi amekufuru aliyoteremshiwa Muhamad S.A.W.
Hadithi ya nne.
عن إبن عباس رضي الله عنه قال قال رسول الله صلي الله عليه وسلم: من إقتبس علما من النجوم إقتبس شعبة من السحر زاد ما زاد (رواه أبو داود وإبن ماجه وغيرهما. قال الحافظ: والمنهي عنه من علم النجوم هو ما يدعيه أهلها من معرفة الحوادث الآتية في مستقبل الزمان ويزعمون أنهم يدركون ذلك بسير الكواكب وإقترانها وإفتراقها وظهورها في بعض الأزمان. وهذا علم إستأثره الله به لا يعلمه أحد غيره.
Amesema Ibn Abbas R.A. amesema Mtume S.A.W.: Mwenye kujitafutia sehemu ya elimu ya nyota basi amejitafutia sehemu ya uchawi, atajizidishia uchawi kadiri atavyojizisia elimu ya nyota. (ameipokea hadithi hii Abu Daud na ibn Majah).
Amesema Imam al-Hafidh al-Mundhiri: Na elimu ya nyota iliyokatazwa hapa ni ile wanayojidai wale wasemao kuwa eti wana elimu hiyo, kwamba wanaweza kutabiri matukio yajayo wakidai eti wanaweza kujua hayo kutokana na mienendo ya nyota (sayari) na michomozo yake ya kukutana au kuepukana na kuchomoza katika baadhi ya nyakati na kupotea nyakati nyengine, na kadhalika. Elimu ya utabiri wa aina hii ni Elimu ya Ghayb ambayo Mwwenyezi Mungu S.W. amejiwekea Yeye Peke Yake na Hakumshirikisha mwengine kuijua. (al-Targhib wa al-Tarhib p.525) Maneno kama hayo vile vile yamesemwa na Maimamu wengi sana kama Imam Nawawi, Ibn Hajar na wengine.
Hadithi ya tano.
عن أ نس بن مالك رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلي الله عليه وسلم: من أتي كاهنا فصدقه بما يقول فقدىبرئ مما أنزل علي محمد صلي الله عليه وسلم ومن أتاه غير مصدق له لم تقبل له صلاة أربعين ليلة (الطبراني)
Amesema Anas bin Malik, amesema Mtume S.A.W.: “ Mwenye kumuendea kahini (mganga, mpiga ramli, mnajimu, mtabiri etc., etc.) na akamuamini anayomuambia basi amejitoa kutokana na aliyoteremshiwa Muhammad S.A.W. Na mwenye kumuendea bila ya kumuamini basi hatokubaliwa swala zake kwa muda wa siku 40.
عن وائلة بن الأسقع رضي الله عنه قالسمعت رسول الله صلي الله عليه وسلم يقول: من أتي كاهنا فسأله عن شيئ حجبت عنه التوبة أربعين ليلة فإن صدقه بما قال كفر رواه الطبراني
Amesema Wa’ila bin al-Asqa’ nimemsikia Mtume S.A.W. akisema: “ Mwenye kumendea kahini (mganga, mpiga ramli, mnajimu, mtabiri, etc., etc.) akamuuliza jmabo basi huondolewa toba (hunyimwa toba) siku arubaini, na akimuamini anayomuambia basi amekufuru”.
عن أبي الدرداء رضي الله عنه قال قال رسول الله صلي الله عليه وسلم: لن ينال الدرجات العلي من تكهن أو إستقسم أو رجع من سفره تطيرا (رواه الطبراني )
Amesema Abu-dard’ai R.A. amesema Mtume S. A.W.: “ Hatopata darja za juu yule ambaye anapiga ramli (anaganga, anatabiri etc., etc.), au anakula kiapo kwenye mizimu, au anafuta safari yake na kurudi kwa kuamini ukorofi”.
عن قطن بن قبيصة عن أبيه رضي الله عنه قال سمعت رسول الله صلي الله عليه وسلم يقول: ألعيافة والطيرة والطرق من الجبت (رواه أبو داود والنسائي وإبن حبان. قال أبو داود: الطرق الزجر والعيافة: الخط أنتهي.
Amesema Qatn bin Qabiswa R.A. kutoka kwa baba yake: Nimemsikia Mtume S.A.W. akisema: “ Utabiri wa michoro, na Utabiri ndege (kusema ndege fulani akiruka kuelekea upande fulani basi kutatokea jambo fulani na akiruka kuelekea upande fulani basi matokeo yake ni jambo fulanif) na Utabiri wa fimbo (utabiri wa kifimbo) yote ni sehemu ya kuabudu asiyekuwa Allah, yaani ni kukufuru.
Hadithi kama hizi ziko nyingi. Mwenye macho haambiwi tazama, mwenye masikio haambiwi sikia, mwenye moyo wa Imani kwa Mwenyezi Mungu hawezi kukana au kupindisha pindisha maneno ya Mtume S.A.W. katika masuala kama haya! Anayetaka kusikia amesikia na asiyetaka kusikia asisikie!
Wa Billah al-Tawfiq
No comments:
Post a Comment