Sunday, February 26, 2012

Iweje Sayyidina Abubakr Sadiq (RA) asimulie hadithi chache?


Je, Unajua?!


Sayyidina Abu Bakr ndiye Swahaba aliyeishi na Mtume S.A.W. kwa muda mrerfu zaidi kuliko Maswahaba wote wengine. Na ndiye aliyeswahibiana na Mtume S.A.W. kwa muda wa uhai wake wote! Lakini, pamoja na hayo yote, ni hadithi chache sana zilizopokelewa kutoka kwake, akimnukuu Mtume S.A.W. Kwanini?!!!


Sayyidina Abu Bakr al-Siddiq R. A. ndiye mwanamume wa mwanzo kabisa kumuamini Mtume Muhammad S.A.W., mara tu baada ya kupewa utume. Aliambatana na Mtume S.A.W. wakati wote huko Makka, kwa muda wa miaka 13 na ndiye aliyefuatana naye kutoka Makka kwenda Madina. Hivyo, ndiye Swahaba wa mwanzo kabisa miongoni mwa
maswahaba wanaume, vile Bi Khadija akiwa ndiye Swahaba wa mwanzo kabisa kuliko mtu yeyote mwengine. Kwa vile Bi Khadija alifariki Makka, kabla ya Hijra, tunaweza kusema kwamba Sayyidina Abu Bakr ndiye mtu aliyaliyeswahibiana na Mtume S.A.W. kwa muda wote wa zaidi ya miaka 23, hadi kufa kwake Mtume S.A.W. Kwa maneno mengine, hakuna Swahaba aliyeishi na Mtume kwa muda mrefu zaidi kuliko Sayyidina Abu Bakr al-Siddiq R.A. Na papo, idadi ya hadithi zilizopokelewa kutoka kwake akimnukuu Mtume S.A.W. ni hadithi 142 tu. Miongoni mwa hizo, hadithi 11 zimo katika kitabu cha Bukhari; moja imo katika kitabu cha Muslim; 6, miongoni mwa hizo, wanashirikiana Bukhari na Muslim na zilizosalia, yaani hadithi 130 zimo katika vitabu vengine vilivyosalia vya hadithi.

Kwanini ikawa hivyo?!!

Jibu ni jepesi sana.

Sayyidina Abu Bakr ameishi na Mtume S.A.W. kwa muda wa uhai wake wote, tokea kupewa utume hadi kufa kwake. Katika muda wote huo, Mtume mwenyewe alikuwepo, na maswahaba wake wote waliokuwa hai, na walikuwa wakipokea mafunzo yao kwa maneno na vitendo kutoka kwa Mtume S.A. moja kwa moja. Hakujakuwa na haja ya Swahaba kuhadithia wengine mafunzo ya Mtume S.A. W. Wote walikuwa wanafunzi wa Mtume S.A.W. Wote walikuwa “ wanakunwa kutoka Gudulia moja”, na UTUME hauna " msemaji rasmi".

Baada ya kufa Mtume S.A.W. Sayyidina Abu Bakr al-Siddiq aliishi kwa muda wa miaka miwili na miezi mine tu, akiwa miongoni mwa Mswahaba wenzake. Mwaka mmoja na nusu wa mwanzo, Sayyidina Abu Bakr al-Siddiq alishughulika kuongoza mapambano dhidi ya watu waliortaddi katika eneo lote la penensula ya Arabia. Kwa maana hiyo, hakujakuweko Waislamu wengi wapya, ambao wangehitaji kusikia Mtume S.A.W. amesema nini kuhusu mambo mbali mbali. Waislamu wepya wameanza kungia katika dini baada ya kusambaa hali ya utulivu katika maeneo ya Waislamu, yaani baada ya vita vya Ridda, ambapo Sayyidina Abu Bakr alifariki miezi kama minane tu baada ya kumaliza fitina hiyo.

Chini ya mwaka mmoja huo, Sayyidina Abu Bak alishughulika zaidi na ujenzi wa dola ya Waislamu na kuanza kutuma baadhi ya Maswahaba wenzake kwenda katika maeneo yaliyokombolewa, mikoani na vitongojini, kwenda kuwafunza watu dini, yeye mwenyewe akisalia Madina, makao makuu ya Dola ya Kiislamu.

Ni katika kipindi hicho cha chini ya mwaka mmoja, ndipo Sayyidina Abu Bakr al-Siddiq alipata nafasi ya ama kuwakumbusha Maswahaba wenzake mafunzo ya Mtume S.A.W. katika mambo ambayo palihitajika ufafanuzi, au aliwaelimisha Waislamu wapya, waliokuja Madina, au aliowaatumia ujumbe huko huko kwao mikonani, yale ambayo yeye mwenyewe ameyasikia kutoka kwa Mtume S.A.W., au amemuona akiyafanya. Ndiyo maana, ni hadithi 142 ndiyo zilizopokelewa kutoka kwake. Radhiya Allahu 'Anhu wa Ardhahu!

Wa billah al-Tawfiq
Dr. A. Shareef

No comments:

Post a Comment