Wednesday, February 29, 2012

Swali kuhusu maana ya Shareef/Sharif


Swali:


Nini maana ya Shareef au Mashareef?
Je, kama ni jina mtu yeyote anaweza kumuita mtoto wake Shareef?
Je, hili ni jina tuu kama majina mengine au inamaana nyingine, au ni ukoo?

Majibu:

Sharif linatokana na Sharaf, lenye maana ya heshima au utukufu. Kwahiyo tunaweza kusema Sharif ina maana ya mheshimiwa kwa tafsiri ya moja kwa moja. Kuna usemi wa kiarabu, "Man sharrafa nafsahu fahuwa shareef" wenye maana kuwa anayejiheshimu ataheshimiwa.



Mtu anaweza kumwita mtoto wake Shareef kama jina lolote lile jengine kuwa ni alama ya kumtambua kijamii. Lakini pia Shareef au Sayyid au al-Habib (singular) Shurafa'a, Saadah au al-Haba'ib ni majina yanayotumiwa na watu, katika sehemu mbali mbali duniani, kumaanisha watu wanaojulikana kuwa ni Ahlul-Bayt, yaani ukoo wa Mtume Muhammad (S.A.W)

Afrika ya Mashariki, Kusini na Misri na Syria, watu wa familia hiyo huitwa: Shareef\Shurafa' au Masharifu kwa afrika ya Mashariki. South Yemen\Hadhramout na Gulf States pamoja na Indonesia na Malaysia wanawaita Sayyid\Saadah au al-Habib\Haba'ib, na kadhalika.

Ahlul Bayt ni vizazi vya watoto wa Sayyidina Ali: yaani Hassan na Hussayn, kupitia Bi Fatma al-Zahraa, binti wa Mtume Muihammad (S.A.W) Mtume S.A.W. aliwakusanya Ali, Fatma na Hassan na Husayn na kutangaza kwamba " Hawa ndio Ahl-Bayt wangu". Kuna hadithi nyingi kuhusu ukoo huo na jinsi ya kutosiwi kupokea zakka au sadaka n.k

Maelezo ya ziada:


Tukirudi kwenye msemo "Man sharrafa nafsahu fahuwa shareef", maana yake ni sahihi kabisa: Matendo ya mtu yanamfanya awe mtu wa kuheshimika au kudharaulika. Bilal bin Rabah (R.A) tunamwita Sayyidina Bilal na tunamuombea radhi za Mwenyezi Mungu kutokana na amali zake nzuri na tumehakikishiwa na Mtume (S.A.W) kuwa Bilal siyo tu ataingia peponi bali ataingia akiwa na mapambo na heshima kubwa. Abu Lahb - ami yake Mtume, damu yake- amelaaniwa na Mwenyezi Mungu ndani ya Qur'ani yeye na mke wake kwa matendo yao maovu! Na ni wazi kuwa ni watu wa motoni licha ya kwamba Abu Lahb ni Ami yake Mtume. Hivyo, nasaba yake haikumfaa kitu. Mwenyezi Mungu anasema: Litapopigwa baragumu hakuna kuulizana nasaba! Na Mtume anasema: Mtu ambaye amali zake hazisogezi mbele basi hawezi kusogezwa na nasaba yake!.

Mwenye kujiheshimu na kujithamini kwa vitendo na amali njema ni mheshimiwa, hata awe nani asili yake. Pale anapotokea mtu mwenye kufungamana na Mtume (S.A.W) kwa damu na akajiheshimu na kutenda mema na kumfuata Mtume (S.A.W) basi anakuwa mheshimiwa maradufu: mara moja kwa matendo yake mema na mara ya pili kwa kuheshimu fungamanisho zake na ukoo wa Mtume (S.A.W) Mwenyezi Mungu tujaaalie miongoni mwa wanamfuata Mtume (S.A.W) kwa maneno na vitendo na wanaoheshimu na kuthamini damu ya Mtume (S.A.W)

Wabillahi Tawfiq

No comments:

Post a Comment