Friday, February 24, 2012

Swali: Kuingia msikitini na kusoma Qur'ani kwa mwenye hedhi...


Swali:

Asalam Alaykum warahmatullahi wabarakatuhu,
Jee, mwanamke akiwa kwenye hedhi anaruhusiwa kwenda msikitini au haruhusiwi?
Na jee, anafaa kusoma Quran kimoyoni au haifai?


Jibu:

Bismillah! Mwanamke awe na hedhi asiwe na hedhi, yeye si najsi. Hivyo basi, hakatazwi kuingia msikitini au kupita msikitini iwapo amejidhibiti vya kutosha ili damu isidondoke na kuangukia kwenye msikiti. Hali
kadhalika, anaweza kusoma Qur'ani kimoyomoyo, kwa wale wanao onelea kuwa hawezi kugusa msahafu, kwa vile hawezi kutawadha. Ama wale wanao onelea kuwa kugusa msahafu siyo lazima uwe na udhu, basi wanasema kuwa anaweza kusoma Qur'ani hata kwa sauti; kwani yeye SI najsi. Zaidi mambo asiyoweza kuyafanya mwenye hedhi ni : Kuingiliana kimwili na mumewe, kama inavyosema aya ya 222 ya Surat al-Baqara; hawezi kusali na wala hatakiwi kulipa; hawezi kufunga lakini anatakiwa kulipa baadaye. Mambo mengine yaliyosalia anayafanya.

Nyongeza; 

Mwanamke aliyeingia katika siku zake, kati kati ya kufanya amali ya Hija au Umra, anaruhusiwa kufanya mambo yote ya Hija au Umra, isipokuwa kusali na kutufu al-Kaaba tu. Mengine yote anaendelea kuyafanya kama haji yeyote yule. Hivyo ndivyo alivyo muelekeza Mtume (S.AW) mkewe Bi Aysha (R.A), baada ya kumuona wakati wakiwa katika Hija amenyong'onyea na kuwa na majonzi, akamuuliza: Je, zimeingia siku zako nini?! Bi Aysha akasema ndiyo. Mtume (S.A.W) akamuambia jidhibiti ipasavyo (jifunge kuhakikisha damu haidondoki nje) na fanya yote anayofanya mwenye kuhiji, isipokuwa kusali na kutufu! Hivyo basi, tunaweza kuelewa kuwa amal zote zilizosalia za Hija au Umra, ikiwa pamoja na kwenda Safa na Marwa, mwenye hedhi anaweza kuzifanya, ilimradi tu amejidhibiti sawasawa asidondoshe damu msikitini. Kama tujuavyo, Safa na Marwa ziko ndani ya Msikiti wa al-Haram. Na hii ni mojawapo ya hoja za wale wenye kusema kuwa mwanamke mwenye hedhi, akisha jidhibiti tu, anaweza kuingia msikitini au kupita msikitini, anaweza kusoma Qur'ani na kadhalika.

Wa billah al-Tawfiq.
Dr. A. Shareef Abdulkader.

No comments:

Post a Comment